SERENGETI, MARA
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amewataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili jambo linalopelekea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
IGP Sirro amesema hayo leo wakati akizindua Ofisi za dawati la jinsia na watoto Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara ambapo wananchi wametakiwakwenda kuripoti matukio ya ukatili hili hatua ziweze kuchukuliwa.
Aidha, IGP Sirro ameendelea kuwaonya wananchi kuacha mara moja vitendovya kihalifu hususani wizi wa mifugo.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Utu wa Mtoto (CDF) bwana Koshuma Mtengete amesema kuwa, ni vyema jamii ikaendelea kuelimika kwa kutoa taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ikiwa ni sambamba na kutokufumbia macho vitendo hivyo.
Kwa upande Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Serengeti ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Nurdin Babu amesema kuwa, wilaya yake imeendelea kutoa elimu kwa kuwaelimisha wananchi hususan kwenye masuala ya kiusalama ikiwemo kuachana na mila kandamizi na zilizokwisha kupitwa na wakati.