Imani potofu yawanyima watoto viziwi elimu ya awali

Na Abby Nkungu, Singida
Tatizo la kukithiri kwa imani potofu
miongoni mwa baadhi ya wananchi kumetajwa kuwa moja ya sababu ya watoto
wengi wenye ulemavu kutokupata elimu ya awali kutokana na kufichwa
majumbani na wazazi au walezi wao bila kuandikishwa shule hadi
wanapokuwa wakubwa.


Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi
Tumaini Viziwi ya mjini Singida, Francis Edward alibainisha hayo wakati
wa mahojiano na Mwandishi huyu juu ya changamoto mbalimbali
zinazojitokeza katika utoaji elimu kwa watoto viziwi.

Alisema kuwa wengi wa watoto hao wenye
mahitaji maalum wamekuwa wakifichwa na wazazi au walezi wao kwa imani
potofu kuwa hawastahili kusoma na kwamba ni aibu mbele ya jamii
inayowazunguka kuwa na mtoto wa aina hiyo; hivyo huwafungia ndani hadi
wanapogundulika wakiwa tayari na umri wa miaka 10 hadi 15.

Alieleza kuwa kulingana na Sera ya elimu
nchini, haiwezekani kumwandikisha mtoto mwenye umri wa miaka 10 au 15
kwenye masomo ya awali; hivyo uongozi wa shule hulazimika kuwavusha
darasa la awali kwa kuwapeleka moja kwa moja darasa la kwanza.

“Hali hiyo inawaathiri kielimu watoto
hao kwa kuwa wanakosa msingi muhimu ambao hutolewa katika Shule za Awali
ili kumjenga mtoto kiakili na kimwili katika kupokea masomo yake ya
madarasa ya juu” alifafanua Mwl Edward.

Alisema kuwa ili kukabiliana na
changamoto hiyo, tayari wameanzisha mpango maalum wa kuwasaka
majumbani watoto viziwi kwa kutumia mbinu na majukwaa mbalimbali katika
kuhakikisha wanaandikishwa darasa la awali wakiwa katika umri mdogo kwa
mujibu wa Sera ya elimu Nchini.

“Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa
shule hii miaka 18 iliyopita, mpango huo umezaa matunda kwa kukusanya
watoto 13 tunaotarajia kuwasajili darasa la awali mapema mwakani”
alibainisha Mwl Edward.

Alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo, Meya
wa Manispaa ya Singida, Gwae Chima alisema kuwa atahakikisha
anashawishi Mamlaka hiyo kuwa na Sheria ndogo na mahsusi kuwabana wazazi
na walezi wenye watoto viziwi ili kuwapeleka shule katika umri mdogo
kujiunga na darasa la Awali huku wadau wa elimu wakiunga mkono hoja
hiyo.

Wadau hao walisema, inasikitisha kuona
katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Sera ya elimu bure na
elimu Jumuishi kwa maendeleo ya elimu kwa wote, bado kuna baadhi ya
wazazi na walezi wanaoendelea kuficha watoto wao jambo ambalo ni
kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Shule ya Msingi Viziwi Tumaini iliyopo
eneo la Karakana mjini Singida ilianzishwa mwaka 2001 na hivi sasa ina
wanafunzi 64 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 2018 ilikuwa
miongoni mwa shule 10 bora Manispaa ya Singida zilizofanya vizuri kwenye
Mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi.