Itigi kukusanya sh bilioni 20 mwaka wa fedha 2020/21

Na Abby Nkungu, Itigi
HALMASHAURI
ya Itigi katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida inakusudia kukusanya
na kupokea zaidi ya Sh bilioni 20.89 kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya
mapato kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Akiwasilisha
Mapendekezo ya Bajeti hiyo mbele ya Kikao maalum cha Baraza la Madiwani
wa halmashauri hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji John Mgalula,
Ofisa Mipango Samwel Sendegeya alisema Sh bilioni 1.96 zitatokana na
vyanzo vya mapato ya ndani wakati zaidi ya Sh bilioni 18.92 zitatokana
na ruzuku ya Serikali Kuu na Wahisani.
Aidha,
alieleza kuwa katika Mpango wa bajeti hiyo ya 2020/21, halmashauri
itajikita zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa
kuongeza ukusanyaji mapato, kuwezesha wananchi kiuchumi, kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi watumishi, miundombinu ya shule na mazingira
ya kujifunzia na kufundishia na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
Pia,
kuboresha huduma za afya kwa makundi maalum, kuimarisha huduma na
upatikanaji dawa na vifaa tiba, kulinda vyanzo vya maji, kuondoa ujenzi
wa makazi holela, kuboresha shughuli za ugani, ufugaji, usalama wa
chakula, kuimarisha na kuendeleza uvuvi, kudhibiti wanyama waharibifu na
uvamizi haramu maeneo ya hifadhi.
 Akijibu
hoja kwa nini halmashauri imependekeza bajeti ijayo kuwa Shilingi
bilioni 20.8 wakati lengo la bajeti inayoendelea (2019/2020) ya Shilingi
bilioni 12.9 tu bado kufikiwa hata nusu yake, Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo, Alli Minja alisema kupandisha bajeti ni namna bora zaidi ya
kupandisha kiwango cha mapato ya halmashauri.
“Kumekuwa
na ulegevu wa ukusanyaji mapato, hilo tutalifanyia kazi safari
hii….tutafanikiwa na kufikia lengo. Matumizi yanaongezeka kila
kukicha, hata mtoto huanza kunyonya, kunywa uji kisha kula ugali. Nasi
hatuwezi kubakia hapo hapo. Hatuna namna, lazima tupandishe bajeti yetu”
alifafanua.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji Bw Mgalula akijibu hoja ya Diwani wa Viti maalum,
Rehema Chizumi juu ya uhaba mkubwa wa watumishi wa kike katika
halmashauri hiyo, alisema njia bora ya kuweza kuwabakisha ni kuweka
mazingira ya kazi na makazi katika hali ya kuvutia ili wasifikirie
kuhamia sehemu nyingine.
“Lakini
Mwenyekiti, mbinu nyingine nzuri ingawa sio rasmi ya kuwafanya
watumishi hawa wa kike wanaokuja kwetu waendelee kubaki nasi ni wananchi
waishio hapa, kuwaoa” alisema kwa mzaha Mkurugenzi huyo huku hoja hiyo
ikiungwa mkono na idadi kubwa ya madiwani.