Jafo akunwa na matumizi na usimamizi wa fedha za miradi halmashauri ya mji mbinga

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji
Mbinga mkoani Ruvuma Grace Quintine wakwanza kulia akiwa na baadhi ya
wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa RUVUMA,Halmashauri Mji
Mbinga imepongezwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman
Jafo kwa usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo
zinazopelekwa katika Halmashauri hiyo.


Na Mwandishi WETU,Mbinga

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo,amemuagiza
mkandarasi Suma Jkt anayejenga jengo la ofisi za Halmashauri ya mji
Mbinga mkoani Ruvuma, awe amekamilisha kazi hiyo ifikapo tarehe 30
Desemba mwaka huu.

Halmashauri ya Mji Mbinga,imeingia mkataba na Suma JKT 
kujenga jengo hilo lenye ghorofa moja kwa gharama ya shilingi bilioni
2.9 mwaka 2018 ili kurahisisha utoaji huduma na kuwaondolea adha
watumishi wa Halmashauri hiyo, ambao kwa sasa wanalazimika kubanana
katika jengo la idara ya ujenzi walilorithi kutoka halmashauri ya wilaya
Mbinga.

Aidha Waziri Jafo, amezitaka  wa Halmashauri nyingine za mkoa
wa Ruvuma,kuiga mfano wa Halmashauri ya mji Mbinga kwa kusimamia
kikamilifu ujenzi wa jengo hilo sambamba na matumizi mazuri ya fedha
zinazopelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
inayolenga kuchochea na kuharasisha maendeleo.

Waziri Jafo ametoka kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati
akikagua ujenzi wa jengo  la ofisi za Halmashauri hiyo na kuwataka
wakurugenzi  wengine wa mkoa wa Ruvuma kuiga utendaji, na uadilifu wa
Mkurugenzi wa Mji Mbinga Grace Quintine na timu yake.

“lazima  wakurugenzi wengine waige mfano mzuri wa Mbinga Mji,
ukipewa fedha basi uzitumie vizuri,Mheshimiwa Rais ametafuta  fedha za
kujenga jengo hili ili watumishi mfanye kazi zenu katika mazingira bora,
Mkuu wa mkoa hapa  nimeridhika na kazi iliyofanyika,kwa kweli
nimefurahi sana kwani fedha zilizoletwa zimefanya kazi  nzuri nampongeza
Mkurugenzi na watu wake”alisema Waziri Jafo.

Waziri Jafo alisema, baadhi ya maeneo zinapelekwa fedha
lakini hakuna kazi zinazofanyika badala yake kunakuwa ubabaishaji mkubwa
unaokwamisha na kuchelewesha mipango ya Serikali.

Ameitak Suma Jkt kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha
jengo hilo linaanza kutumika kabla ya mwisho wa mwezi Januari 2020  kwa
kuwa mkataba  wake ni Mwezi Desemba 2019 na imani yake kuwa watumishi
watahami  katika jengo hilo mapema.

Kwa upande wake mhandisi anayesimamia ujenzi wa jengo hilo
Amos Agostine alisema, ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 95 na
kwamba gharama za ujenzi ni zaidi ya  Bilioni 2,983,122,246.

Amos alisema, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho
kukamilisha ujenzi huo kwa kupaka rangi,kuunganisha umeme,kujenga ngazi
na shughuli nyingine ndogo ndogo.