Jaji mkuu: msikubali kuingiliwa katika mamlaka zenu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwaapisha Mahakimu Wakazi wa
Mahakama za Mwanzo wapya  leo Novemba Mosi, mwaka huu katika ukumbi
namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Salaam, Mhe Beatrice Mutungi.
Mahakimu Wakazi wa Mahakama za
Mwanzo wapya wakila kiapo cha kuitumia kazi yao leo Novemba Mosi, mwaka
huu, katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo
jijini Dar es Salaam.
Picha na Magreth Kinabo- Mahakama
……………..
Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amewaasa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya
kutokubali maelekezo ya aina yoyote kutoka nje ya Mamlaka zao kuhusiana
na mashauri yaliyopo mbele yao.
Akizungumza na Mahakimu Wakazi hao
,wapya 23 mara baada ya kuwaapisha rasmi, mapema Novemba 01, 2019
katika Ukumbi wa Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu
alisema kuwa Mahakimu hao wana mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri
bila kuingiliwa na yeyote.
“Jaji au Hakimu lazima awe ni mtu
wa kuheshimu mamlaka nyingine, vivyo hivyo msikubali maelekezo ya aina
yoyote kutoka nje ya Mahakama ama iwe Jaji au mtu mwingine kuhusiana na
kesi/mashauri yaliyopo mbele yenu,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.
Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa
kuwataka Mahakimu hao kutekeleza majukumu yao bila upendeleo kwa kuwa ni
jambo linalosababisha matabaka baina ya watu/wananchi.
“Upendeleo ni jambo la hatari
sana, muwe wawazi, muwe wasikilizaji makini, lazima muwasaidie wananchi
ambao wengi hawajui sheria kwa kuwaelimisha,” alisisitiza Mhe. Jaji
Mkuu.
Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu
aliwapa angalizo Mahakimu hao juu ya uandishi wa hukumu sahihi kwa
kutumia lugha inayoeleweka ili wananchi/wateja waweze kuelewa kwa
urahisi.
Masuala mengine aliyowaeleza
Mahakimu hao ni pamoja na kufanya tafiti, matumizi ya TEHAMA na kuishi
viapo vyao wanapotekeleza majukumu yao. 
Jumla ya Mahakimu Wakazi wapya 23
wameapishwa na wamepangiwa kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo katika
mikoa mbalimbali nchini