Serikali yawatoa hofu wananchi wa handeni mkoani tanga

Serikali
imewahakikishia wakazi wa Handeni, Mkoani Tanga uendelevu wa huduma ya
maji licha ya kuharibika kwa miundombinu ya maji kulikosababishwa na
mvua zinazoendelea kunyesha.


Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa kauli hiyo
hapo juzi wilayani hapa wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua athari
ya mvua kwenye miundombinu ya maji sambamba na kupata ufumbuzi wa haraka
kufuatia hali ya mvua zilizonyesha kwa takribani wiki mbili mfululizo.

Mara
baada ya kujionea hali halisi, Mhandisi Sanga aliwatoa hofu wananchi wa
Handeni ambapo aliwataka kuwa watulivu na aliahidi kuwa Serikali
itahakikisha huduma ya maji inarejea haraka iwezekanavyo.

“Ninawasihi wananchi kufanya subira na kuwa watulivu na kuzingatia maelekezo ya Serikali,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi
Sanga alibainisha kuwa zoezi la tathmini ya athari ya mvua hizo kwenye
miundombinu ya maji wanaloendelea nalo halitochukua zaidi ya siku tatu
kama ilivyoagizwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.

“Waziri
wa Maji ametuagiza kuharakisha kukamilisha zoezi hili, nasi
tutahakikisha linafanyika kwa kasi ikiwa ni pamoja na kutazama njia
mbadala ili wananchi wapate huduma ya maji kwa haraka,” alisema Mhandisi
Sanga.

Aliongeza
kuwa Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli haipo tayari kuona wananchi
wake wanataabika na kwamba hatua madhubuti na za haraka zinachukuliwa
ili kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Awali
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela akielezea kwa ujumla athari za
mvua hizo kwenye Mkoa wa Tanga, alisema kuwa zimeleta madhara kwenye
miundombinu ya barabara na madaraja na kusababisha huduma ya usafiri
katika maeneo mbalimbali kuathirika.

“Tulichokibaini
katika mvua hizi zilizonyesha ni kuwa zimeharibu mabwawa ya maji na
kusababisha maji yaliyotoka katika mabwawa hayo kuathiri miundondombinu
mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara,” alieleza Shigela.

Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe akielezea athari
za mvua hizo alisema ni pamoja na kuharibika kwa mabwawa 11 ya maji
yanayotumiwa na wakazi wa Handeni na maeneo jirani na kati ya hayo yapo
mabwawa makubwa matano ambayo aliyataja kuwa ni Kwenkambara, Mandera,
Suwa, Msomera na Mkomba.

Aidha,
Gondwe alipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt.
John Pombe Magufuli kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa wakati na
kwa hatua mbalimbali za haraka zinazoendelea kuchukuliwa ikiwa ni
pamoja na kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara na maji
iliyoathirika.

Sambamba
na hilo, Gondwe alimpongeza Mhandisi Sanga na timu ya wataalam
aliyoambatana nayo kutoka Wizara ya Maji na taasisi zake kwa kufika
Wilayani hapa mapema ili kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya
mabwawa ya maji ili kupata ufumbuzi.

“Kwa
niaba ya wananchi wa Wilaya ya Handeni tunatoa shukrani nyingi sana kwa
Mheshimiwa Rais kwa kutujali na kuwatuma watendaji wa Serikali kufika
hapa Handeni ili kutatua matatizo yaliyosababishwa na mvua kubwa
zilizonyesha,” alisema Gondwe.

Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA),
Mhandisi Clement Kivegalo ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Sanga
alisema kuwa wanaendelea na tathmini ila kwa mabwawa yaliyopasuka
wamebaini yalijengwa chini ya kiwango na pia hayakuwa yakitunzwa
inavyostahili na hivyo kupelekea kuharibika wakati mvua hizo
zilizonyesha.