Kamati yaziagiza wma na wrrb kuendelea kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma

 

Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) (wa
kwanza kushoto) akipitia mawasilisho wakati wa semina iliyolenga
kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini
Peter Mwita Getere, akichangia katika semina iliyolenga kuwaelimisha
wajumbe wa Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu
utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini
Dodoma.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa WMA, Bi.
Stellah Kahwa (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji WRRB Bw. Asangye
Bangu (watatu kutoka kushoto wakiwa katika semina iliyolenga
kuwaelimisha wajumbe wa Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira
kuhusu utekelezaji wa majukumu ya WMA na WRRB iliyofanyika Bunge jijini
Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeagiza Wakala wa Vipimo (WMA)
na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuendelea kuboresha
utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Hayo, yalisemwa na
Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na
Mazingira Mhe. Erick Shigongo (Mb) wakati wa semina iliyolenga
kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
WMA na WRRB na mafanikio yake iliyofanyika Juni 24, 2021 katika ukumbi
wa Bunge jijini Dodoma.

Naye, Naibu Waziri
wa Viwanda Mhe. Exaud Kigahe (Mb) akijumuisha maoni na mapendekezo ya
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira
alisema Serikali imepokea maoni yote na itayafanyia kazi ili kuboresha
huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Nao, Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira walitoa
maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma na bidhaa
zinazotolewa na WMA na WRRB ikiwemo Matumizi ya mizani, upimaji wa
mafuta, utunzaji wa mazao katika maghala, na utoaji wa stakabadhi
ghalani.

Akiwaelimisha
Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa WMA, Bi. Stellah Kahwa
alisema WMA inajukumu kubwa la kumlinda Mlaji na umma kwa ujumla kwa
Kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kwenye Sekta za Biashara, Afya,
Usalama na Mazingira, Kukagua usahihi wa bidhaa zilizofungashwa na
kudhibiti udanganyifu wowote wa kivipimo (Ukaguzi na Udhibiti) na
Kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ili kuilinda jamii iweze kuepukana na
madhara yatokanayo na matokeo ya matumizi na upimaji usio sahihi katika
“Biashara, Afya, Usalama na Mazingira.

Bi. Kahwa pia
alisema Wakala hutekeleza majukumu yake ya ukaguzi kwa kusogeza huduma
kwa wateja wake kwa kutumia vituo vya muda 5,030 kote nchini (Tanzania
bara) katika ofisi za Kata, Mitaa na Vijiji. Aidha, huwahudumia wenye
vipimo visivyohamishika kama pampu za mafuta, mizani za Barabarani,
Viwanda, waagizaji na wafungashaji mahali walipo.

Aidha, Bi Kahwa
alisema kuwa WMA ina Kituo kikubwa cha kisasa kilichopo misugusugu
kinachotumika kupima matenki yabebayo mafuta, Dira za Maji na Dira za
Umeme. Huduma hizo zinapatikana katika vituo saidizi vilivyopo mikoani.

Naye Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji WRRB Bw. Asangye Bangu aliwaelimisha wajumbe hao
kuhusu majukumu ya WRRB kusema kuwa WRRB ina jukumu la kutoa leseni za
uendeshaji wa ghala pamoja, kusimamia maghala hayo pamoja na kuhamasisha
utumiaji wa Mfumo wa stakabadhi za ghala nchini kwa kushirikiana na
sekta binafsi na Taasisi za umma zinazosimamia mazao na bidhaa
zinazoweza kutumika katika Mfumo wa stakabadhi ghalani.