Kambi za kujisomea kuongeza uelewa kwa watoto

Na MWANDISHI WETU-MONDULI  

WENYEVITI wa Vitongoji na Vijiji wilayani Monduli
mkoani Arusha wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kutoa elimu kwa wazazi juu ya
umuhimu wa kupeleka watoto kwenye kambi za kujisomea.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi
Kimanta wakati wa ziara ya kutembelea na kuzindua makambi 10 mapya kati ya 14
yaliyoanzishwa mwaka 2017-2018 chini ya uratibu wa Shirika la World Vision
Tanzania (WVT).
  Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta akionyesha baadhi ya vitabu    wanavyotumia wanafunzi kusoma wakiwa kwenye kambi za kujisomea 


Mradi wa kufungulia usomaji unalengo la kuimarisha
kujifunza kusoma na kuandika unatekelezwa katika vijiji vitatu vya Esilalei,
Mswakini na Mtimmoja chini ya Mradi wa Kisongo Makuyuni (AP).

Akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi wa kambi za
usomaji Shule ya Msingi Laiboni, Esimiti,Endepesi, RC Kanisani, Engasiti, Kanisani,
Shuleni, Noongojio na Megwara Kimanta alisema, kambi hizo zinakuza sekta ya
elimu hivyo ni muhimu zikapewa kipaumbele na jamii.

“Kazi ya kuwawezesha watoto kujua kusoma na kuandika
ni ya serikali, lakini hapa inafanywa na World Vision kama wadau wa sekta ya
elimu kipekee wanstahili kupongezwa kutokana na mchango wao katika shughuli za
maendeleo wilayani kwetu,” alisema Kimanta na kuongeza:

“Nawaagiza Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji
kuhakikisha mnazitambua kambi zote za usomaji zilizoanzishwa na WVT. Lakini pia
kuhakikisha wazazi wanapeleka watoto kusoma,” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Monduli mkoani Arusha Iddi Kimanta mwenye (fulana) akiagana na wazazi wa Mtaa wa Megwara ilipo kambi ya usomaji kwa wanafunzi  

DC Kimanta katika hatua nyingine aliitaka jamii
kuangalia namna ya kuwawezesha walimu wanaojitolea kufundisha watoto muda wa
Saa 3 kwa siku za Jumamosi  kuwawezesha
fedha za nauli na chakula.

Msimamizi wa Mradi wa Elimu Kisongo Makuyuni (AP),
Steward Mwilenga alisema program ya usomai ilianza kutekelezwa mwaka 2017
nchini baada ya matokeo chanya ya mradi wa majaribio wa “Watoto Tusome” wa
mwaka 2013-2016 uliotekelezwa Kisongo, Magugu na Mtinko Singida.

Mwilenga aliyataja mafanikio ya utekelezaji wa mradi
huo kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha darasa la 1 hadi 3
juu ya mbinu mbalimbali za ufundishaji ambapo jumla ya walimu 26 walijengewa
uwezo.

Msimamizi wa Mradi wa Elimu Kisongo Makuyuni (AP), uliopo chini ya ufadhili wa Shirika la World Vision Tanzania (WVT), Steward Mwilenga akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta.

“Walimu nane wa kiume na 18 wa kike kwa sasa
wanaendelea kuutumia madarasani. Kwa sasa tunakabiliwa na changamoto moja ya
mwitikio mdogo wa baadhi ya wanajamii juu ya umuhimu wa makambi ya kujisomea
kwani mahudhurio ya watoto yamekuwa hafifu,” alisema Mwilenga.

Baadhi ya shughuli zinazotekelezwa na mradi wa
kufungulia usomaji ni pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika makambi na
mashuleni ili kubaini mafanikio na changamoto.Kununua vitabu vya darasa la 1-3
vyenye maudhui ya kuongeza ujuzi wa kujua kusoma na kuandika.

Nyingine ni ujenzi wa madarasa ya awali ili kupunguza
adha ya upungufu wa madarasa mashuleni pamoja na kujengea uwezo waratibu elimu,
wadhibiti ubora wa shule na maafisa taaluma juu ya kushauri na kufundisha.

Naye Afisa Elimu wilaya ya Monduli Theresia Kyara aliwapongeza
World Vision kwa kuja na mradi huo huku akiwataka viongozi waliopata fursa ya
kwenda kujifunza namna makambi ya usomaji yanavyofanya kazi mkoani Tanga
kutimiza wajibu wao.

Aidha Mwenyekiti wa Makambi Kijiji cha Esilalei Nailenya
Mapi Meshuko alisema ushiriki wa wazazi katika eneo hilo umeanza kuwa na
mwitikio unaoridhisha kutokana na kuwa na idadi ya wanafunzi zaidi ya 200.
Mwenyekiti wa Kambi za usomaji Kijiji cha Esilalei Nailenya Meshuko mwenye shati jeupe akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta.

Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta akikagua baadhi ya majengo ya madarasa na Vyoo vya kisasa katika Shule ya Msingi Laiboni yanayojengwa na Shirika la World Vision Tanzania (WVT)

Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddi Kimanta akiwa nje ya jengo la Choo cha kisasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika Shule ya Msingi Laiboni.