Kampuni ya barrick gold yaahidi kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika tanzania

Ofisa
mtendaji mkuu wa kampuni ya Barrick Gold,  Dk Mark Bristow amesema
kampuni hiyo itajifunza kwa makosa iliyoyafanya nchini Tanzania miaka 10
iliyopita.


Dk
Bristow ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 Ikulu jijini Dar
es Salaam katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya
Tanzania na kamati ya madini ya Barrick.

 
Amesema
tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani kumekuwa na safari ndefu ya
majadiliano kati ya kampuni hiyo na Serikali yaliyowezesha kugawana
mapato sawa.

“Sisi
wawekezaji tunapokuja kwenye nchi kama hii tuna jukumu kubwa la
kuchimba rasilimali ya Taifa si kwa faida yetu tu bali kwa faida pia ya
Taifa na wadau wengine. Wadau hao siyo tu wanahisa, bali wananchi ndiyo
maana ni wajibu wetu kulipa kodi.”

“Vilevile
siyo tu kwa Watanzania wa sasa bali pia vizazi vijavyo vina haki ya
kupata mgawo. Kuna jamii zinazozunguka migodi, lazima zishiriki shughuli
za uchumi,” amesema.

Baada
ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali
ziliunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini
ya kampuni ya Acacia.