Katibu mkuu ccm awataka wapinzani wajiandae kukubali kushindwa

Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amevitaka vyama vya
upinzani nchini kujiandaa mapema kukubali kushindwa kama ambavyo CCM
ilikubali kushindwa katika baadhi ya majimbo mwaka 2015.


Ameeleza
kuwa CCM ikishindwa huwa inakubali kushindwa kama ambavyo walikubali
mwaka 2015 katika majimbo mbalimbali nchini ikiwemo jimbo la Kigoma
Mjini, hivyo amevitaka vyama vya upinzania navyo viige mfano huo wa CCM
na waanze mapema kujiandaa kukubali kushindwa.

Katibu
Mkuu ameyasema hayo, jana tarehe 17 Januari, 2020 alipokuwa akizungumza
katika mkutano wa ndani na wajumbe wa mikutano mikuu ya kata, kamati ya
siasa ya wilaya ya Uvinza, Waasisi, wazee maarufu, wenyeviti wa
mashina, mabaraza ya Jumuiya ngazi ya matawi na kata, wenyeviti wa
vijiji na serikali zao, Kata ya Kazuramimba wilayani Uvinza Mkoa wa
Kigoma.

“wanaCCM
tukishindwa hukubali kuwa tumeshindwa, tuliposhindwa Kigoma Mjini
Ubunge na Halmashauri tulikubali na wao wajifunze pia kwamba
unaposhinda, unayemshinda akubali na kuwa muungwana kuwa umemshinda, na
akirudi awamu nyingine akakung’oa na wewe ukubali”.

Amesisitiza
kuwa, “Nimekuja kutoa ujumbe Kigoma nzima, ikiwemo Kigoma Mjini kuwa,
tumejipanga kushinda, wajiandae kukubali kushindwa, hivyo nimekuja
kufunga mitambo ya ushindi wa maendeleo na kwa hali ya Kigoma ni lazima
nifunge mitambo ya kimkakati, ndio maana nilianza Unguja, Pemba,
nikaenda Tanga na kisayansi ilinitaka ndani ya masaa 48, niwe nimefunga
Kigoma na nimefanya, kwa kuwa jana nilikamilisha Tanga, leo nimeifunga
rasmi hapa”.

Aidha,
katibu Mkuu pamoja na mambo mengine, amesisitiza uimarishaji wa
Serikali za Mitaa ambapo amegusia baadhi ya sifa za wanachama wa CCM
watakaowania nafasi za Udiwani ni lazima wawe ni watu ambao tutaamini
wanaweza kuongeza tija katika maendeleo ya watu, wenye uelewa juu ya
maisha ya watu, kwa kuwa serikali za mitaa ni kiungo muhimu kwa
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Diwani
wa CCM ni lazima awe na uelewa wa maisha ya watu na hii haihitaji
shahada, inahitaji uelewa na ushirikiano na wananchi wenzake, wanamjua
vizuri, anawajua vizuri anayajua mazingira vizuri, yupo tayari, je
atatumika au anakwenda kutumikiwa? Ni lazima tuwe na uhakika
atatufikisha mbali , hata Mbunge naye ni Diwani hivyo ni lazima awe na
sifa za kiungo, na atatumika vizuri kwenye Baraza kuunganisha
halmashauri na masuala ya kitaifa”.

Mkutano
huo wa ndani umehudhuriwa na wanachama wa CCM na viongozi mbalimbali wa
Chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma Ndg.
Amandus Nzamba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ndg. Kirumbe Ngenda,
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga,
Mbunge wa Jimbo la Uvinza Bi. Hasna Mwilima, Mbunge wa Viti Maalum Bi.
Zainabu Katimba na Mkuu wa wilaya ya Uvinza Ndg. Mwanamvua Mlindoko.