Katibu mkuu hazina ahimiza watumishi wa tra kuongeza bidii ukusanyaji mapato

Veronica Kazimoto na Rachel Mkundai
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amewahimiza
watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kufanya kazi kwa
bidii, weledi, na kwa kuzingata misingi wa Sheria za kodi ili
kuhakikisha kuwa TRA inaendelea kuvunja rekodi ya makusanyo ya mapato
kama ilivyokuwa katika mwezi Septemba na Desemba, 2019.

Pia,
amewapongeza watumishi wote wa Mamlaka hiyo kwa kujituma na kupelekea
Serikali kukusanya mapato kiasi cha Sh. trilioni 9.341 sawa na ufanisi
wa asilimia 47.67 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 19.595 kwa mwaka wa
fedha 2019/2020 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019/2020
yaani kuanzia Julai hadi Desemba 2019.

Akizungumza
wakati wa mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka
2019/20 wa Mamlaka hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha, Bw.
James alieleza kuwa, mapato makubwa yanayotegemewa na Serikali ni
makusanyo ya kodi ambapo aliwaasa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa
bidii na weledi ili kuongeza mapato na hatimaye Serikali iweze
kutekeleza mipango yake iliyojipangia ya kuwaletea wananchi wake
maendeleo.

“Ukiangalia
mchanganuo wa makusanyo yote ya Serikali, sehemu kubwa sana ni kodi
inayokusanywa na TRA. Kwa msingi huu, TRA inapofanikiwa kukusanya kodi
kwa ufanisi mkubwa ndiyo mafanikio ya Serikali katika kutekeleza bajeti
inayokuwa imepangwa kwa kipindi hicho,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Aidha,
aliwashukuru wananchi na walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa
hiari na wakati ambapo makusanyo ya mwezi Septemba na Desemba, 2019 ni
ishara kwamba, walipakodi kwa ujumla wao, wanaunga mkono juhudi za
Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza mapato ya ndani na pia
wameendelea kutambua umuhimu wa kulipa kodi baada ya kuona utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini inayofanywa na Serikali yao.

“Tunawashukuru
sana walipakodi wa nchi hii kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa
kuisadia Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi hiyo
kubwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo. Kitendo hiki kiendelee na
ikiwezekana iwe zaidi ya hapo”, alieleza Bw. James.

Akizungumzia
suala la mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji mapato, ukiwemo mfumo wa
mnada wa forodha kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu huyo, ameipongeza TRA
kwa kuendelea kuboresha mifumo hiyo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa
kuongeza mapato ya Serikali.

“Mfumo
wa mnada wa forodha kwa njia ya mtandao ni mfumo mmojawapo kati ya
mifumo mingi inayotumiwa na TRA katika kukusanya mapato. Mfumo huu,
ambao umejengwa na Watalaam wetu wa TRA, umeonesha mafanikio makubwa kwa
sababu unashirikisha watu wengi na kuleta ushindani wa haki kwa wote.

“Ni
matarajio yetu kuwa, Serikali itapata mapato yake stahiki kutokana na
kuuzwa kwa bidhaa zilizokaa muda mrefu bandarini tofauti na matakwa ya
Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
ya mwaka 2004 na ni matumaini yetu kwamba, kuuzwa kwa wakati kwa bidhaa
hizo kupitia mfumo huu, kutapunguza mrundikano wa bidhaa bandari na
hivyo kuongeza ufanisi wa bandari zetu na vituo vingine vya forodha”,
alieleza.

Hata
hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James
amewaagiza viongozi wa TRA kufanya maboresho ya mifumo ndani ya Mamlaka
hiyo mara moja pale watakapobaini mapungufu yoyote ambayo yanaweza
kukwamisha utendaji kazi wa mfumo husika.

Kwa
upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede, alisema kwamba,
mkutano huo wa mapitio na tathmini ya nusu mwaka ulilenga kufanya
maboresho katika utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa malengo
waliyopangiwa na Serikali yanafikiwa.

Dkt.
Mhede aliongeza kuwa, TRA imepewa agizo na Serikali la kukusanya kiasi
cha sh. trilioni 19.5 katika mwaka huu wa fedha 2019/20 ambapo pamoja na
kufanya vizuri katika miezi ya Septemba na Desemba, 2019, alikiri kuwa
bado Mamlaka hiyo haijafikia malengo ya makusanyo kwa asilimia 100.
Hivyo, mkutano huo ulilenga kufanya marejeo na maboresho ya mikakati ya
utendaji kazi itakayowezesha kufikia malengo hayo kwa asilimia 100.

“Kupitia
Sheria ya Bajeti, SURA 439, TRA tumepewa agizo na Serikali la kukusanya
mapato kiasi cha sh. trilioni 19.595 hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020
na wakati tukitekeleza robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha
2019/2020, hatukufanikiwa kufikisha asilimia 100 ya makusanyo ya robo
hizo. Hii ndiyo moja ya sababu tumeona tukutane ili tubaini maeneo yenye
mapungufu na kisha tufanye marejeo shirikishi ili tujisahihishe na
kuweka mikakati itakayotuwezesha kufikia lengo”, alisema Dkt. Mhede.

Mkutano
wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa TRA
ulihudhuriwa na jumla ya washiriki 361 ukihusisha Menejimenti nzima ya
Mamlaka, Mameneja wote wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania Bara na
Visiwani pamoja na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.

Washiriki
wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wawakilishi kutoka
baadhi ya Asasi za Serikali kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mfuko wa Bima ya
Afya (NHIF), Ofisi ya Rais – Tume ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mganga
Mkuu – Mkoa wa Arusha, na Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAeSA)
iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira) ambapo kwa siku ya
kwanza wawakilishi wa Asasi hizo walitoa maada kuhusu masuala
mbalimbali ya kuisaidia TRA kuongeza makusanyo ya Serikali.