Katibu mteule tsc aanza kazi rasmi

 

Mwenyekiti wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba (kushoto),
akimkaribisha Katibu Mteule wa Tume hiyo, Mwl. Paulina Nkwama katika
Ofisi yake mpya, Makao Makuu ya Tume, Dodoma, baada ya kuripoti rasmi na
kuanza kazi, Aprili 1, 2021.

Mkurugenzi wa
Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC),
Moses Chitama (kulia), akimkabidhi Katibu Mteule wa Tume, Mwl. Paulina
Nkwama, Ripoti kuhusu Tume husika, wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha
Ofisini kwake, Makao Makuu Dodoma, baada ya kuripoti rasmi na kuanza
kazi, Aprili 1, 2021.

Katibu Mteule wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama, akiendelea na
majukumu Ofisini kwake, Makao Makuu Dodoma, muda mfupi baada ya kuripoti
rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.

Katibu Mteule wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama (aliyesimama),
akizungumza na Wajumbe wa Menejimenti, Makao Makuu Dodoma, muda mfupi
baada ya kuripoti rasmi na kuanza kazi, Aprili 1, 2021. Kulia kwake ni
Mwenyekiti wa TSC, Prof Willy Komba na kushoto kwake ni aliyekuwa Kaimu
Katibu, Moses Chitama.

Watumishi wa Tume
ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wakimpokea Katibu
Mteule wa Tume hiyo, Mwl. Paulina Nkwama, alipowasili kuanza kazi rasmi,
Aprili 1, 2021.

Mkurugenzi wa
Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC), Christina Hape (kushoto), akiwasilisha salamu za
ukaribisho kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote, kwa Katibu
Mteule wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama (kulia), baada ya kuripoti rasmi
Makao Makuu Dodoma na kuanza kazi, Aprili 1, 2021.

Mkurugenzi
Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Tume ya Utumishi wa Walimu
(TSC), Shani Kamala, akiwasilisha Taarifa kuhusu Tume kwa Katibu Mteule
wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama (hayupo pichani), alipokutana na Menejimenti
baada ya kuripoti rasmi Makao Makuu Dodoma na kuanza kazi, Aprili 1,
2021.

Katibu Mteule wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama (kushoto),
akimshukuru kwa kumfikisha salama na kuagana na aliyekuwa Dereva wake,
Sajenti Martin Mwanandota, baada ya kuripoti rasmi Ofisi yake mpya,
Makao Makuu Dodoma, Aprili 1, 2021. Kabla ya uteuzi wake, Mwl. Nkwama
alikuwa Katibu Tawala Msaidizi (Elimu), Mkoa wa Kilimanjaro.

Veronica Simba na Adili Mhina

Katibu Mteule wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwalimu Paulina Nkwama, leo Aprili 1,
2021 ameripoti Ofisini kwake, Makao Makuu ya Tume, jijini Dodoma na
kuanza kazi rasmi.

Mwl. Nkwama
ameanza majukumu yake baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo
kuanzia Machi 29 mwaka huu, akichukua nafasi ya Winfrida Rutaindurwa
ambaye amemaliza muda wake.

Akizungumza na
Menejimenti ya TSC, muda mfupi baada ya kuwasili ofisini hapo, Mwl.
Nkwama amesisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa
watumishi ili kwa pamoja waweze kutimiza azma ya kuihudumia vyema kada
wanayoisimamia, yaani Walimu walio katika Utumishi wa Umma.

“Kwenye Taasisi
kukiwa hakuna upendo ni changamoto, hivyo nawaomba tupendane,
tushirikiane na tushikamane. Tukienda hivyo, naamini kwa msaada wa
Mungu, tutafanikiwa.”

Aidha, Katibu
Mteule Nkwama ametumia nafasi hiyo kueleza shukrani zake kwa Mwenyezi
Mungu kwa kumwezesha katika hatua mbalimbali za maisha yake hadi kufikia
mahali alipo na pia amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumwamini na
kumteua kushika wadhifa husika.

“Naamini
Mheshimiwa Rais aliwaona wengi ambao wana sifa za kushika wadhifa huu,
lakini akaniamini mimi na kunipa nafasi ya kuwatumikia Watanzania
hususani Walimu ambao Tume hii inawasimamia. Namshukuru sana na
ninaahidi sitamwangusha,” ameeleza Mwl. Nkwama.

Vilevile,
amewataka watumishi wote wa TSC kutambua kuwa yeyé ni mtumishi mwenzao
hivyo waachane na kasumba za kumwogopa kutokana na wadhifa wake. Badala
yake amewataka wawe huru kushirikiana naye katika kazi huku akiahidi
kupokea ushauri kutoka kwa yeyote na kuufanyia kazi ili kupata matokeo
chanya.

Kwa upande wake,
akimkaribisha Katibu Mteule, Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba
amempongeza kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kushika nafasi hiyo.

Aidha, Prof.
Komba amemweleza Katibu Mteule Nkwama kuwa Menejimenti ya TSC ina
Wajumbe mahiri wenye weledi na utendaji mahiri wa kazi, hivyo anaamini
kupitia uongozi wake, Tume itaendelea kufanya kazi nzuri.

Akizungumza
katika hafla hiyo fupi ya ukaribisho, aliyekuwa Kaimu Katibu wa TSC,
Moses Chitama ameeleza kuwa Tume imepokea uteuzi wa Mwl. Nkwama kwa
furaha kubwa na kwamba wana imani naye.

Akizungumza kwa
niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote, Mkurugenzi wa Idara ya Ajira,
Maadili na Maendeleo ya Walimu Christina Hape, ameahidi kuwa watampatia
ushirikiano Katibu Mteule ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi.

Awali,
akiwasilisha Taarifa fupi kuhusu TSC kwa Katibu Mteule, Mkurugenzi
Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Shani Kamala, alibainisha
jukumu kuu la Tume kuwa ni kuendeleza na kusimamia Utumishi wa Walimu.

Kabla ya uteuzi
wake, Mwl. Nkwama alikuwa Katibu Tawala Msaidizi (Elimu), Mkoa wa
Kilimanjaro. Zoezi la kuapishwa kwake linatarajiwa kufanyika siku yoyote
kutoka hivi sasa baada ya taratibu husika kukamilika.