Na Claud Gwandu,Arusha
KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Arusha limetoa ofa ya kufanyiwa ukaguzi na Matengenezo ya magari bure kwa muda wa wiki mbili katika Chuo cha Ufundi Magari na Gereji ya Kanisa hilo inayosimamiwa na Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria iliyopo Ungalimited,jijini hapa.
Ofa hiyo kwa wenye magari ilitangazwa juzi na Paroko wa Parokia hiyo,Padre Festus Mangwangi wakati wa uzinduzi wa Chuo hicho kinachoitwa Chuo cha Ufundi Magari na Gereji cha Mtakatifu Gabriel uliofanywa na Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isaac Amani.
Uzinduzi wa Chuo hicho na gereji chenye wanafunzi 53,kumi wakiwa wa kike. ulienda sambamba na uzinduzi wa Chuo cha Ushonaji cha Parokia hiyo ambacho kina wanafunzi 48.
Akizungumza katika uzinduzi huo,Padre Mangwangi alisema kuwa ofa hiyo ya ukaguzi wa bure wa magari ni sehemu ya mkakati wa Chuo hicho kusaidia wenye magari wanaohitaji msaada wa kiufundi
“Tumekarabati Chuo chetu kwa gharama ya zaidi ya sh milioni 150 kwa kuweka vifaa na zana za kisasa za ufundi hivyo tutafanya ukaguzi bure lakini wenye magari watalazimika kununua vipuri chuoni na vipuri vyetu ni vya kutoka kwa watengenezaji halisia (original) na vya kisasa.
“Baada ya ofa ya wiki mbili za ukaguzi bure kumalizika,tutatoa ofa ya wiki mbili nyingine za kulipia nusu ya gharama kwa wenye magari,hii yote ikiwa ni msaada kwa jamii tunayoitumikia,” alisisitiza Padre Mangwangi.

Baba Askofu Mkuu Amani aliwataka vijana wanaopata nafasi ya kusoma chuoni hapo kuonyesha mfano wa umahiri na kujifunza kwa bidii na nidhamu ili wakawe mfano wanapomaliza mafunzo yao.
Chuo hicho kinatoa kazi mbalimbali za ufundi magari kwa miaka mitatu kwa kadiri ya maelekezo ya Msajili wa Elimu ya Ufundi Stadi(VETA) na chuo kimefanikiwa kuwa na walimu na wanafunzi wa fani zote tatu za ufundi zinazotolewa chuoni hapo.
Fani hizo ni pamoja na Ufundi Magari,Ufundi wa kuchomea ,kunyoosha na kupaka rangi magari na fani ya umeme wa magari.

APC