Lema alia na utekaji, ataka wananchi, taasisi kupaza sauti

Egidia Vedasto
Arusha

Wananchi na Tasisi mbalimbali za kijamii zimetakiwa kupaza sauti zo kwa kukataa vitendo vya utekaji vinavyoendelea nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Arusha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Kaskazini Godbless Lema amewashauri wananchi kuacha kushabikia Simba na Yanga na badala yake kujikita katika mambo ya msingi yenye mustabakali wa maisha yao.

“Mko wapi Mashekhe, Maaskofu na Wachungaji? Mko wapi Wasanii na wananchi wengine mnaoguswa na matukio haya yanayotishia uhai wa wananchi wasio na hatia? amehoji na kuendelea.

“Nawaambia msijifariji hali ni mbaya na tunakoenda ni kubaya zaidi, watoto, vijana wanatekwa, wengine wanaokotwa wamekufa lakini cha kushangaza hakuna kauli ya Serikali yenye majibu kwa nini matukio ya namna hii yanazidi kuongezeka, watu kupoteza wapendwa wao” amesema Lema.

Kwa upande wake Mchungaji wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Kati Usharika wa Olosiva Ibrahim Loivotoki Jijini Arusha amesema kwa upande wake kama Kiongozi anayeongoza kundi kubwa la watu jukumu lake ni kuhubiri amani, upendo mshikamano na utulivu katika jamii.

Pia ameiomba Serikali kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika wakijihusisha na vitendo vya ubakaji, ulawiti na utekaji ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma na kuweka amani na utulivu kwa wananchi.

“Niwakumbushe wananchi kutoa taarifa na ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi mnapobaini vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu katika jamii zetu zinazotuzunguka na tuwe na hofu ya Mungu siku zote ili itubidishe kupendana” amesema Mchungaji Ibrahim.

Mama mmoja mkazi wa Kata ya Moshono ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema vitendo vya utekaji ni uvunjifu wa amani, hivyo Serikali iwajibike kukomesha vitendo hivyo ili wananchi waendelee kujenga uchumi wao.

“Sasa hivi tunaishi kwa hofu kubwa, watoto wanatekwa, watu wanachinjwa wanatolewa viungo hali inatisha na inatia hofu, Serikali tunataka majibu juu ya wanaotekwa na kuuawa” amesema .