Maafisa ugani arusha wapewa mafunzo ya kukabiliana na nzige

 

Na Mwandishi wetu Arusha

Shirika la
chakula duniani (FAO) kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo wamefanikiwa kutoa
mafunzo ya kupambana na nzige  wa jangwani kwa maafisa ugani 42 wa mkoa wa
Arusha lengo likiwa ni kujiandaa kupambana na nzige ambao hufanya uharibifu wa
mazao na mimea mbalimbali.

Akizungumza
mapema jana wilayani Monduli mara baada ya kufunga mafunzo kwa maafisa ugani wa
wilaya ya Monduli Afisa afya ya mimea kutoka FAO, Mushobozi Baitani alisema
kuwa tahadhari ya Nzige hao ni muhimu kuchukuliwa

Baitani
alisema kuwa janga la Nzige ni janga ambalo ni baya sana na linaathari kubwa
sana kwenye jamii ndio sababu wameanza kuchukua tahadhari kwa kuanza kuwapa
mafunzo wataalamu hao wa Mkoa wa Arusha

Alidai kuwa Nzige
wanapovamia mahali huwa wanatabia ya kuharibu vyakula,mazao,pamoja na malisho
mbalimbali ya mifugo jambo ambalo linasababisha ukame kwenye jamii husika
ambayo hutegemea zaidi kilimo

“Athari
za Nzige hawa wa jangwani kwa kweli ni kubwa sana na madhara yake ni makubwa
sana sasa nchi kama Tanzania tayari tumeshaanza kuchukua tahadhari kwa kutoa
mbinu na mikakati mbalimbali ya kupambana na Nzige hao endapo kama watavamia
maeneo mbalimbali”aliongeza

Katika hatua
nyingine alisema kuwa jitihada mbalimbali ambazo wamezifanya ni pamoja na kutoa
elimu sanjari na vitendea kazi kwa maafisa ugani hao ili endapo kama Nzige hao
wa jangwani watawasili waweze kukabiliana nao ipasavyo ikiwa ni pamoja na
kiangamiza kizazi chao chote.

Katika hatua
nyingine alisema kuwa kwa nchi ya Tanzania mpaka sasa haijavamiwa na nzige hao
wa jangwa ambao wametokea ukanda wa jangwa la sahara wakaingia somalia na kisha
kuingia nchi za kenya na uganda

Alidai kuwa
upepo wa Nzige hao wa jangwani upo nchini kenya na uganda lakini huenda ifikapo
November mwaka huu upepo ukabadili njia na kisha tatizo la nzige kuwa
limekwisha kabisa kwa kuwa kizazi cha kwanza kilishamalizika

Alihitimisha
kwa kusema kuwa Nzige hao sio janga jepesi kabisa hivyo basi maafisa hao ugani
wanatakiwa kutumia mafunzo hayo vyema lakini pia FAO kwa kushirikiana na wizara
ya Kilimo wanampango wa kuendelea kutoa mafunzo kwa maafisa ugani hasa wa mikoa
ya mipakani kwa ajili ya tahadhari zaidi.