Makala – serikali kuongeza bajeti utafiti wanyapori

  • Tanapa, Tawiri kushiriki utafiti
    wanyamapori waliotoweka

  •   Yafanikiwa kurejesha Mbwa mwitu hifadhi
    ya Serengeti

Seif Mangwangi
MBWA Mwitu ni miongoni
mwa wanyamapori ambao wanaelezwa kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka duniani
kufuatia kuuawa kwa wingi pamoja na kukumbwa na magonjwa hatari. Hivi sasa
wanyama hawa wanapatikana katika nchi saba pekee duniani ambazo ni Tanzania,
Kenya, Botswana, Zimbabwe, Zambia, Afrika Kusini na Lesotho.
Tishio la kutoweka kwa
wanyama hao nchini lilijitokeza mwaka 1994 baada ya kundi la mwisho kuondoka
katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kukimbilia kwenye makazi ya watu jirani
na hifadhi hiyo.
Mbwa mwitu ambao
nchini pia hupatikana katika hifadhi za Ruaha na pori la Akiba la Selous na
mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, wanaelezwa kukimbia ndani ya hifadhi ya
Serengeti baada ya wengi wao kufa kufuatia kukumbwa na ugonjwa wa kichaa cha
mbwa pamoja na Kichaa cha Simba ‘Canaid Center virus. Hata hivyo huko
walipokimbilia pia huuawa kwa wingi kufuatia kula mifugo ya wanavijiji.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prf Jumanne Maghembe akikata utepe kuashiria
kuachiliwa kwa mbwa mwitu kundi la sita ndani ya hifadhi ya Serengeti, watatu kulia kwake ni Balozi wa
Ujerumani nchini Egon Karionke na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijazi. (PICHA NA
SEIF MANGWANGI)

Hata hivyo Shirika la
Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa kushirikiana na mashirika mengine ikiwemo
taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI), waliamua kushirikiana
kutafiti sababu ambazo zimepelekea kutoweka kwa wanyama hao.
Kwa mujibu wa Mtafiti
Mwandamizi katika taasisi ya utafiti wanyamapori Tawiri, Dkt Eblate Mjingo,
baada ya kutoweka kwa wanyama hao, mwaka 2005 waliamua kufanya utafiti na
hatimaye waliweza kugundua kuwa Mbwa Mwitu hao walitoweka baada ya kukumbwa na
magonjwa ya kichaa cha mbwa na kichaa cha simba.
“Mbwa mwitu ni mnyama
muhimu sana katika hifadhi hasa Serengeti yenye wanyama wengi, ambao wamekuwa
na kazi moja tu ya kupunguza idadi ya wanyama kwa kuwa wao ni wanyama wanaokula
nyama,”anasema.
Anasema baada ya
kugundua tatizo lililopelekea kutoweka kwao ndani ya hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, timu ya watafiti ikaamua kujenga eneo maalum la kuwahifadhia wanyama
hao na kuanza kuwakamata kutoka katika maeneo ya jirani na kuwaweka katika eneo
hilo kabla ya kuwaachia na kutawanyikia porini.
 “Kundi la kwanza tulianza kulitoa mwaka 2012
baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, tunachokifanya hivi sasa ni kuwavalisha
mikanda inayoendeshwa kwa kutumia satellite hivyo tunakuwa tunajua kila baada
ya saa moja wanakuwa wapi,”anasema.
Anasema mikanda hiyo
yenye uwezo wa kusoma GPS, hutumika kutambulisha wanyama hao maeneo
wanayopendelea kutembea na endapo watatoka nje ya hifadhi watajulikana
wameelekea wapi na hivyo kuwatafuta na kuwarejesha hifadhini.
Akizungumza katika
hafla ya kufungulia kundi la sita la Mbwa Mwitu hao, katika eneo la Nyansori
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,  aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Professa Jumanne Maghembe amesema idadi yao imeongezeka na kufikia 120.
Mtafiti Mkuu Mwandamizi wa taasisi ya utafiti wanyamapori (TAWIRI), Dkt Eblate Mjingo
akizungumza na mwandishi wa makala hii, Seif Mangwangi kuhusu utafiti wa Mbwa mwitu unaofanyika
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti. (PICHA NA SEIF MANGWANGI)
Kundi hilo lenye idadi
ya mbwa mwitu 17 imelezwa kuwa wamekaa katika eneo hilo la hifadhi kwa
takribani miezi sita kwa lengo la kuwazoesha mazingira ya Serengeti kabla ya
kuachiwa.
Hata hivyo Maghembe
anasema Serikali itaongeza bajeti ya utafiti wa wanyamapori ikiwemo utafiti wa
Mbwa Mwitu ili kurejesha mfumo wa ekolojia wa wanyama hao ulioanza kupotea na
kusababisha kutoweka kwa baadhi ya makundi ya wanyamapori nchini.
Anasema bila utafiti
wa wanyamapori na kugundua changamoto zinazowakabili sehemu kubwa ya wanyama
hao wataendelea kutoweka na kubakia kuwa historia huku Serikali ikipoteza fedha
nyingi za kigeni zinatotokaa na uwepo wa wanyama hao.
“Tunaendelea kukusanya
fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi na katika bajeti ijayo tutaongeza
fedha kwaajili ya wanasayansi katika utafiti wa wanyamapori ili kurejesha
vizuri mfumo wa ekolojia wa wanyama hao ikiwemo mbwa mwitu na kuwaokoa katika
hatari ya kutoweka, pia tutaongeza idadi ya watafiti na vifaa vya
kutosha,”anasema.
Professa Maghembe
anasema kiasili kila mnyama ameumbwa kwa malengo fulani na ndio maana kuna
wanyama wanaokula majani na wanyama wanaokula nyama na hivyo kuwafanya kila
mmoja kuwa na faida yake.
“Kila mnyama ndani ya
hifadhi amekuwa na faida yake, hawa mbwa mwitu wamekuwa na faida kubwa katika
mfumo wa ekolojia ambapo kazi yao kubwa ni kula wanyama wenzao ikiwemo
waliozeeka, endapo hawatafanya hivyo wanyama wataongezeka na kumaliza malisho
yaliyokuwepo,”anasema.
Professa Maghembe
anasema Wizara ya Maliasili na utalii sio ya kuipuuza kwa kuwa imekuwa
ikiingizia Serikali pato kubwa linalofikia asilimia 17 na kwamba ukijumuisha na
misitu inafikia asilimia 20 kwa mwaka.
Meneja mradi huo wa
utafiti wa Mbwa Mwitu kutoka taasisi ya Tawiri, Emanel Masenga anasema Mbwa
mwitu katika hifadhi ya Serengeti wamekuwa wakitunzwa na kulishwa mbuzi ambao
hununuliwa kutoka kwa wafugaji waliokuwa jirani na hifadhi ya Serengeti.
Anasema mbuzi ambaye
hulishwa Mbwa mwitu hao, huchunwa ngozi ili kuondoa harufu itakayotambulisha
aina ya mnyama anayeliwa na hivyo kumuepusha na mazoea kuwa anakula mbuzi jambo
ambalo linaweza kusababisha wakakimbilia vijijini na kuanza kushambulia mbuzi.
Kwa siku mbwa mmoja hula kilo nne za nyama na kukaa siku moja kabla ya kula
tena.
Masenga anasema
wamekuwa wakiwakamata mbwa mwitu hao kutoka katika maeneo ya jirani kwa
kuwapiga sindano za usingizi kisha kuwapakia katika magari na kuwafikisha ndani
ya eneo lililotengwa kwaajili ya kuwatunza.
“Kwa kawaida
tunamuacha mnyama aishi maisha ya kiasili lakini kwa hawa tumelazimika
kuwarejesha sababu wanatoweka, sehemu ya Makundi ya Mbwa Mwitu yamekimbilia
vijijini, tunachofanya ni kuwakamata kutoka katika maeneo hayo na kuwahifadhi
kwa miezi sita katika eneo maalum lililozungushiwa uzio kuzuia wasitoroke kabla
ya kuwaachilia,”anasema na kuongeza:
“Hivi sasa tuna idadi
ya mbwa mwitu 120 ndani ya hifadhi ya Serengeti, kupitia makundi sita
yaliyokuwa yameshahifadhiwa hapa ndani 
hii ni faraja sana kwetu kwa kuwa baadhi ya watalii hupenda kuangalia tu
wanyama hawa, sasa wakikosekana ni hasara kwa Taifa kwa kuwa tunakuwa hatujamfurahisha
mtalii,”anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi anasema utafiti huo wa mbwa
mwitu unaofanywa na taasisi ya utafiti wa wanyamapori nchini (TAWIRI),
utasaidia kuepusha migogoro na wananchi kufuatia makundi ya mbwa mwitu
kutorokea katika eneo la Loliondo na kuanza kula mbuzi na kondoo.
Anasema pia kuachiliwa
kwa Mbwa mwitu hao na kuwarejesha katika maeneo yao ya  asili ni msaada mkubwa kwa Serikali kwa kuwa
watasaidia kurejesha mfumo wa ekolojia na kuongeza utajiri wa wanyamapori ndani
ya hifadhi ya Serengeti.
Mtafiti Mkuu
Mwandamizi kutoka taasisi ya Tawiri Dkt Eblate Mjingo anasema hivi sasa kuna
Mbwa mwitu mmoja miongoni mwa kundi hilo la sita amezaa hivyo wanaendelea
kumuhudumia katika kituo hicho kabla ya kumuachilia.
Maisha ya Mbwa mwitu
Mtafiti Eblate Mjingo
anasema kwa kawaida Mbwa mwitu ambao huishi katika makundi huweza kubeba mimba
mara mbili kwa mwaka na mimba hiyo hukaa kwa siku 70 kabla ya kujifungua. Pia
huzaa kati ya watoto 12 hadi 18 kwa mara moja. Hata hivyo katika kila kundi
Mbwa mwitu mmoja pekee ndio hubeba mimba.
Kundi la Mbwa Mwitu waliokuwa wamehifadhiwa katika eneo maalum ndani ya hifadhi ya
Taifa ya Serengeti wakikimbia kuingia porini ndani ya hifadhi hiyo baada ya kuachiliwa. ( PICHA NA SEIF
MANGWANGI).
Anasema maisha ya Mbwa
mwitu hutegemeana na eneo analoishi ambapo endapo akiishi maisha ya kiasili
huishi miaka 6 hadi 7 lakini akiishi maeneo yaliyotengwa na kufuatiliwa (zoo),
huishi hadi kufikia miaka 10 tangu kuzaliwa.
Mjingo anasema Mbwa
mwitu ambao kiasili ni mnyama mpole kwa binaadam wamekuwa wakivutia katika
uwindaji ambapo humkimbiza mnyama na kuanza kumla kwa kumdonoa huku akiwa
anaendelea kukimbia au kasimama.
“Mbwa mwitu humla
mnyama akiwa katika harakati za kukimbia, hufanya hivyo kwa sababu hawana uwezo
wa kumuangusha mnyama hivyo hugawanyika makundi matatu, kundi la kwanza
husimama kulia kwa mnyama na la pili kushoto kwake wakiendelea kumla huku kundi
la mwisho likifanya ulinzi kuhakikisha wanamtisha mnyama asikimbie,”anasema.
Hata hivyo utafiti wa
Mbwa mwitu unaelezwa kuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha za utafiti,
vifaa kama magari na kwamba hali hiyo imekuwa ikisababishwa na namna ambavyo
jamii imekuwa ikipokea mradi huo kufuatia kufanywa na watanzania wenyewe.
Utafiti huo hugharimu Milioni 150 kwa mwaka.
seifmangwangi@gmail.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *