Makonda awataka watumishi wa serikali kuwahudumia kwa haki na usawa

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu wa Siasa,uenezi
na mafunzo  wa Chama Cha Mapinduzi CCM
Taifa Mhe. Paul Makonda amewataka watumishi wa Serikali kuwahudumia Wananchi
kwa haki na usawa  na kwamba
watakaobainika kushindwa kuwahudumia
wananchi hawatavumiliwa.

Ameyasema hayo leo Jumapili Januari 28,2024 kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Town mjini Shinyanga
ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza viongozi kutimiza wajibu wao kwa
wananchi wote bila kujali hali zao.

Mhe. Makonda ametahadharisha watumishi hao wa serikali wanaoshindwa kuwahudumia
wananchi, kutetea na kulinda maslahi yao ambapo amesema kipaumbele chake ni
kuhakikisha wananchi wote wanahudumiwa kwa haki na usawa.

Pia ameonya kuhusu watumishi wanaotumia vyeo vyao kuminya haki za
wananchi na kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

“Yule anayeonea watu anayethurumu watu anayetumia cheto chake bila kujali
utu huyo sitakuwa sehemu yake na kwa namna hii naomba niwaambie watumishi wa
serikali wote wa ngazi zote, ukiharibu Chama hiki cha Mapinduzi msemaji wake ni
Makonda siwezi kukutetea utabeba mzigo wako mwenyewe”.

“Kwahiyo kama kuna mtumishi amezoea kuwanyima haki wananchi kama kuna
mtumishi hawathamini wananchi kama waajili wake CCM ya Samia haitambeba na
msemaji wake ni Makonda nitafanya kwa mujibu wa sheria”.
amesema Mhe. Makonda

Katibu huyo pamoja na mambo mengine amesikiliza na kutatua kero za
wananchi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kwenye mkutano
huo  ambapo wamemshukuru na kumpongeza
kwa hatua hiyo ya kusikiliza changamoto zao.

Katibu wa Siasa,uenezi
na mafunzo  wa Chama Cha Mapinduzi CCM
Taifa Bwana Paul Makonda leo ametatua changamoto za wananchi wa Mkoa wa
Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mikoa mbali mbali Nchini ambapo
jana alikuwa  Wilayani kahama na kwamba
Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa wa 9 katika ziara zake.

Aidha mkutano
umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Dini, Vyama vya siasa, viongozi wa
kimila pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Christina Mndeme, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi, Kamanda wa jeshi
la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi, Mbunge
wa Jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi, Mbunge wa jimbo la
Msalala Mhe. Idd Kassim, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga pamoja na wataalam
kutoka idara mbalimbali.