Egidia Vedasto,
APC media, Arusha.
Asasi za Kiraia Nchini (AZAKI) zimeandaa jukwaa la elimu linalolenga kuyapa nafasi makundi yote ndani ya jamii kuweza kushiriki katika michakato yote ya kidemokrasia nchini ikiwemo uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Arusha Mkurugenzi wa nchi (CBM) Kimataifa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Wiki ya Cso Anesia Mahenge amesema zaidi ya watu 600 nchi nzima watashiriki katika maadhimisho hayo ambapo jukwaa litaangazia elimu kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Ikumbukwe jukwaa kama hili hufanyika kila mwaka, na mwaka huu tuna mambo mengi mbele yetu hivyo ni muhimu kushirikishana kikamilifu ili kupata fulsa za Uongozi na Utawala bora kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu” amesema Mahenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa AZAKI Justice Rutenge ameeleza kwamba, kuelekea kipindi hiki cha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na uchaguzi ujao ni vema Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu wainuke na kutumia fulsa hizo kugombea nafasi mbalimbali za uongozi badala ya kupiga kura tu na kutolewa maamuzi.
“Kazi yetu ni kuhakikisha kuna ujumuishi wa sekta zote hasahasa watu walioko pembeni kwa lengo la kupaza sauti zao ambazo ndio msingi wa jukwaa letu”amefafanua Rutenge.
Mkurugenzi Mtendaji katika Programu ya mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi ameeleza kuwa jukwaa hilo linalenga makundi yote kupaza sauti zao hususan wanawake wa kimasai na wale walioko pembezoni.
“Tunatarajia kuangazia maeneo ya uwekezaji kwa wanawake, kigoda cha vijana na masuala ya ukatili, uchumi na maendeleo yao” amesema Liundi.
Sambamba na hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Bora Ishmail Biro, amesema vijana ndio lengo kuu na majukumu ya AZAKI ni kuhamasisha utawala bora, uchumi na ajira stahiki.
“Kijana ndiye mtekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na wanatakiwa kushiriki michezo mbalimbali ili kuweka afya zao vizuri na kubadilishana mawazo chanya ya kujenga taifa na katika jukwaa hili litakalodumu kwa siku tano tumeandaa michezo mbalimbali ambayo tunategemea vijana wajitokeze kwa wingi maana jukwaa ni lao” ameeleza Biro.
Pia Mkuu wa Sekta ya Umma katika Benki ya Stanbic Nchini Doreen Dominic ametoa wito kwa Taasisi zingine za Kifedha kutoa ushirikiano katika majukwaa mbalimbali kama njia ya kuiunga mkono Serikali.
“Benki yetu ni ya kwanza Afrika na ya tatu kwa Tanzania katika kuisapoti AZAKI katika kutimiza malengo yao ya kuinua uchumi wa mwananchi wa hali ya chini na matarajio yetu ni kuona yale yote yatakayowasilishwa yanafanyiwa kazi” ameeleza Dominic.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki elimu John Kalage amefafanua kwamba ushiriki wa vijana katika michakato ya Kidemokrasia ni hafifu, hivyo jitihada zinatakiwa ili kuwafanya vijana kujua wajibu wajibu wao katika masuala hayo.
“Tunataka Vijana waongezewe ujuzi maono na weledi wa kuongozakuongoza, washiriki kikamilifu kuandaa Sera ya Maendeleo ya Taifa” amesema Kalage.
Kwa upande wake Mshauri wa Kimkakati Prudence Zoe Glorious ameeleza kwamba siku tano za jukwaa zitasheheni malumbano ya hoja, ushauri na maoni mbalimbali ili kuongeza thamani katika nchi.
“Jukwaa la Wiki ya AZAKI litajadili mabadiliko ya tabia ya nchi, nafasi ya mwanamke wa Kimasai pamoja na kilinge cha vijana” ameeleza Prudence.
Wiki ya AZAKI ni ya sita tangu kuanzishwa kwake, itadumu kwa siku tano Jijini Arusha imebeba kaulimbiu ya “Sauti, Dira na Thamani” na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo.