Mbunge sangu aiomba serikali kuchunguza unyanyasaji wanaofanyiwa wananchi na magereza mollo sumbawanga

Na Alex Sonna, Dodoma.


Mbunge
wa Kwela kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Deus Sangu ameishauri
Serikali kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza unyanyasaji unaofanywa na
Askari wa Jeshi la Magereza Mollo Sumbawanga kuhusu tamko la Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi la kutoa shamba lenye ukubwa wa Ekari 495 kwa
wananchi wa vijiji vya Msanda Muungano, Songambele na Sikaungu


Katika
maswali yake ya nyongeza bungeni wakati wa maswali na majibu, Mhe.
Sangu amebainisha kuwa Jeshi la Magereza linasema halijapata barua rasmi
kutoka Wizarani.


“Tamko
hili limesababisha askari Magereza sasa kuingia mgogoro na wananchi na
kuwapiga na juzi mama mmoja amepigwa na kugalagazwa kwenye matope,
je,Wizara ipo tayari kuunda tume kuchunguza manyanyaso haya na
itakapobainika hatua za kisheria zichukuliwe ili iwe fundisho kwa
wengine,” amesema.


Aidha
ameiomba Serikali kutimiza ahadi ya kukabidhi shamba lililokuwa
limechukuliwa na Jeshi la Magereza Mollo Sumbawanga kwa wananchi na
Waziri wa Mambo ya ndani kwa wakati huo aliahidi kukabidhi shamba hilo
kwa wananchi.


Akijibu
swali hilo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamza Khamis Khamis,
amesema Wizara itachunguza na ikibainika kuna watu wanahusika hatua
kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Aidha
amebainisha kuwa Jeshi hilo na wananchi wa vijiji hivyo walikuwa na
mgogoro ambao ulimalizwa Mwaka 2019 kwa Serikali kutoa eneo la ekari
1,800 kwa lengo la kumaliza mgogoro huo.


Amesema
kuwa hitaji la ekari 495 ni dai jipya ambalo Wizara kwa kushirikiana
na Jeshi la Magereza na Ofisi ya Mkoa wa Rukwa litaendelea kulifanyia
kazi.