Mchungaji kanisa la baptist apandishwa kizimbani akituhumiwa kujeruhi kwa viboko waumini wake kama sehemu ya maombezi na toba kanisani kwake

Mchungaji wa Kanisa la Baptisti Milton Wikunge akisindikizwa kwenda mahabusu baada ya kushtakiwa kwa kosa la kujeruhi waumini wake ikiwa ni katika kutekeleza ibada ya maombezi katika kanisa hilo

Na Joctan Agustino,Njombe 
MCHUNGAJI wa Kanisa la Baptisti na mkazi wa kijiji cha Mawindi, Milton Wikunge(56) pamoja na
Nolbat Mbude mkazi wa Igima wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe
wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe leo oktoba 21 kujibu mashtaka ya  kujeruhi waumini watatu katika
kanisa hilo.

Akisoma mastaka yanayowakabili watuhumiwa hao
mwendesha mashtaka wa serikali Hapness Makungu amesema watuhumiwa
wanakabiliwa na makosa matatu ya kujeruhi kinyume na Kifungu cha sheria
225 cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu no 16 marejeo ya 2002 ambayo
waliyafanya oktoba 13 kwa watu watatu ambao wadaiwa kuwa ni waumini wa
kanisa hilo ambao ni Elesi Fwami,Shahibu Mhema na Regina Lyahumi.

Watuhumiwa
wote wamekana kuhusika na tuhuma hizo za kujeruhi jambo ambalo
limefanya mahakama kupitia kwa hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa
wa Njombe Iluvan Msaki kuahirisha kesi hiyo hadi octoba 31 itakapotajwa
tena kwa lengo la kuendelea na uchunguzi zaidi.

APCBLOG  
imezungumza na mkuu wa wilaya ya Wangingombe Comrade Ally Kassinge
anakiri kutokea kwa matukio hayo ambapo amesema kwa taarifa za awali
inaonyesha watuhumiwa walitoa adhabu ya viboko kwa waumini hao kwa lengo
la kuwapa toba ya makosa waliyatenda na kuwasabishia majeraha makubwa
kwa muumini anaetambulika kwa jina la Elisia Fwime ambaye amelazwa
hospitali ya Kibena wilayani Njombe .

Kufuatia hali hiyo mkuu
huyo wa wilaya anasema amejipanga kufanya ziara wilaya nzima kwa lengo
la kutoa elimu kwa wananchi kupinga vitendo vya imani potofu ikiwemo ya
kanisa linalotuhumiwa kuwaadhibu waumini wao ili kutubu dhambi zao.

Watuhumiwa
wote wawili ambao ni viongozi wa kanisa hilo walitiwa nguvuni na vyombo
vya dola baada ya kukutwa na tuhuma za kuwaadhibu waumini wao watatu
viboko na kusababisha majeraha makubwa kwa lengo la kuwapa toba jambo
ambalo limepingwa vikali na serikali wilayani humo.

Katika hatua
nyingine watumiwa hao wameshindwa kupata dhamana ambayo inagharimu Tsh mil 3
kutokana na wadhamini wao kukosa barua kutoka kwa mtendaji wa kata.