Mganga wa kienyeji ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mtoto wa miaka 8

Mahakama
ya Wilaya Kigoma Mkoa wa Kigoma imemhukumu mganga wa kienyeji, Venas
Edward (48), mkazi wa Ujiji Manispaa ya Kigoma/Ujiji kutumikia kifungo
cha maisha jela kwa kosa la kumnajisi mtoto wa kike mwenye umri wa miaka
minane.



Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Katoki Mwakitalu,
baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka
yoyote.

Hakimu
Mwakitalu alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa
ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Raymond Kimbe, na ulipeleka mashahidi
wanne na kielelezo kimoja ambacho ni PF3.

Alisema
mama wa mtoto huyo alimpeleka mtoto wake nyumbani kwa mshtakiwa kwa
ajili ya kutibiwa, na baada ya kumfikisha, mganga alimtuma mama huyo
aende dukani kununua wembe.

Alisema baada ya mama kwenda dukani, mshtakiwa alimfanyia mtoto huyo kitendo hucho cha kikatili.

Alieleza kuwa baadaye mama wa mtoto huyo alifika kutoka dukani na kumchukua mtoto wake na kurudi nyumbani kwake.

Alieleza
zaidi kuwa baada ya muda mama alisikia mtoto wake analalamika kusikia
maumivu sehemu zake za siri, ndipo mama alipomkagua na kugundua kuwa
mtoto wake alikuwa amenajisiwa.

Aliendelea
kueleza kuwa mama wa mtoto huyo alimbana mtoto wake kwa kumuuliza ni
nani aliyekufanyia kitendo hicho ndipo alimjibu kuwa ni mshtakiwa.

Mshtakiwa
huyo baada ya kuhukumiwa kwenda jela maisha, aliangua kilio hadharani
na kusababisha ndugu zake nao kuanza kuangua vilio mahakamani mbele ya
umati uliofika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo.

Awali
akisoma hati ya mashtaka Wakili Kimbe alidai kuwa Aprili 23, mwaka 2019
majira ya asubuhi eneo la Kasoko Ujiji, mshtakiwa alinajisi mtoto huyo
na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.