Minada ya forodha sasa kufanyika kwa njia ya mtandao

 Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede akizungumza
na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati
akitangaza kusitisha rasmi minada ya hadhara ya forodha iliyokuwa
ikifanyika hapo awali na badala yake minada hiyo itakuwa ikifanyika kwa
njia ya mtandao kupitia Tovuti ya TRA ambayo ni 
www.tra.go.tz na tarehe 2 Januari, 2020 kutakuwa na mnada huo utaofanyika kwa njia ya mtandao.
 Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza
kusitisha rasmi minada ya hadhara ya forodha iliyokuwa ikifanyika hapo
awali na badala yake minada hiyo itakuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao
kupitia Tovuti ya TRA ambayo ni 
www.tra.go.tz na tarehe 2 Januari, 2020 kutakuwa na mnada huo utaofanyika kwa njia ya mtandao.
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kusitisha minada ya hadhara ya
forodha iliyokuwa ikifanyika hapo awali na badala yake minada hiyo
itakuwa ikifanyika kwa njia ya mtandao kupitia Tovuti ya TRA ambayo ni 
www.tra.go.tz.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka hiyo Dkt. Edwin Mhede amesema kwa mara ya kwanza, mnada kwa njia
ya mtandao utafanyika tarehe 2 Januari, 2020 ambapo kutakuwa na
ushindani wa haki na taarifa zote za washindi zitaonekana kwa uwazi
kwenye tovuti hiyo ya TRA.
“Napenda
kuwataarifu rasmi kuwa, kuanzia sasa mamlaka itafanya minada yote kwa
njia ya mtandao na kwa kuanzia tutakuwa na mnada mnamo tarehe 2 Januari,
2020.
“Hivyo,
nachukua fursa hii kuwaalika wananchi wote walioko ndani na nje ya nchi
kushiriki mnada huo na ninawakumbusha kuwa, bado wana haki ya kukagua
bidhaa kabla ya kununua kwa wale watakaoweza kufika kwenye maeneo bidhaa
zilipo”, alisema Dkt. Mhede.
Dkt.
Mhede ameyataja mafanikio ambayo TRA inayatarajia kutokana na mfumo huu
mpya ambapo amesema ni pamoja na bidhaa nyingi zinatarajiwa kuuzwa kwa
wingi na hatimaye makusanyo ya kodi yataongezeka.
Pia,
watanzania wengi wenye nia watapata fursa ya kununua bidhaa bila
kuongeza gharama kwa kutumia madalali na wanunuzi watakuwa na muda wa
kutosha wa kununua bidhaa hizo huku kukukiwa na ushindani wa haki.
Mafanikio
mengine ni kupungua kwa gharama zinazotumiwa na mamlaka kuendesha
minada kulinganisha na utaratibu uliokuwepo hapo awali na hivyo kazi hii
itafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Kamishna
Mkuu Mhede alieleza jinsi ya kushiriki mnada kwa njia ya mtandao ambapo
alisema kuwa ni lazima mshiriki awe na kifaa chochote chenye mtandao
popote alipo kama vile simu ya mkononi, kompyuta au kompyuta mpakato.
Vilevile,
ni lazima mshiriki awe amejisajili kwenye mfumo na kwa wale wasiokuwa
na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) watatakiwa kujisajili kwa
kuwasilisha taarifa zao kwenye mfumo ili kupata TIN kwanza.
Baada
ya kuingia kwenye tovuti, mshiriki atachagua bidhaa mbalimbali na
kuanza kushindana na washiriki wengine kwa kuweka bei na atakuwa na
uwezo wa kuongeza bei kadri ushindani utakavyokuwa ukiendelea.
Aidha,
mshiriki atakayekuwa ameshinda atataarifiwa kwenye mfumo na anaweza
kupata ankara kwa ajili ya kufanya malipo na hatimaye mshindi atapata
hati ya kuruhusu mzigo kutolewa maeneo ya forodha kwa njia hiyo hiyo ya
mtandao.
Awali,
Kamishna Mkuu huyo Dkt. Edwin Mhede alizitaja changamoto za mnada wa
hadhara uliokuwa ukifanyika zamani kwamba, ulikuwa ukifanyika mara moja
kwa wiki na hivyo kusababisha bidhaa kutokuuzwa kwa wakati na kupelekea
serikali kutokukomboa kodi yake kwa wakati.
Pia,
washiriki wa mnada walikuwa ni walewale na wengi wao walikuwa siyo
wanunuzi huku wakiingilia minada na kufanya wanunuzi wenye nia kushindwa
kununua bidhaa.
Changamoto
nyingine ilikuwa ni ulipaji wa malipo ya awali ya asilimia 25 kwa
washindi ulikuwa ukihitaji washindi hao kwenda eneo la mnada na fedha
taslimu na kwa wale wanaolipa kwenye akaunti zao iliwalazimu wawe na
akaunti ya benki iliyopo kwenye eneo la mnada wakati kwa sasa mshindi
hulipia mzigo kupitia kwenye akauti yake kwa kutumia ankara na
halazimiki kwenda TRA isipokuwa wakati wa kuchukua mzigo wake tu.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania imeamua kubadilisha mfumo wa kufanya mnada wa
hadhara wa forodha ikiwa ni sehemu ya kuondokana na changamoto
zilizokuwepo kabla ya kuanza kwa mfumo wa kielektroniki, kutekeleza
Mpango Mkakati wa Tano wa TRA na Mpango Kabambe wa Serikali ya Awamu ya
Tano wa kuwa na Serikali Mtandao ambapo Wizara, Idara, Wakala na Taasisi
za Serikali zinatakiwa kuendesha shughuli zake hasa za ukusanyaji wa
Mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.