Mkurugenzi nec aahidi kushirikiana na waandishi wa habari uchaguzi mkuu 2020

Mwenyekiti wa Arusha Press Club, Claud Gwandu akimkabidhi cheti cha shukrani Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, Dkt Wilson Mahera ikiwa ni utambuzi wa mchango wake kwa wanahabari alipokuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha DC.
Mkurugenzi wa NEC Dkt Wilson Mahera akisaini kitabu cha wageni
Mkurugenzi wa NEC Dkt Wilson Mahera akisalimiana na baadhi ya waandishi na wanachama wa APC mara baada ya kupokea cheti cha heshima kutoka kwa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKURUGENZI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt Wilson Mahera
amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya
habari nchini kuelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Akizungumza wakati wa hafla fupi, ya kukabidhiwa cheti cha
kutambua ushirikiano wake na waandishi wa habari alipokuwa mkurugenzi wa Halmashauri
ya Arusha DC, Dkt Mahera ametoa shukrani kwa waandishi na vyombo vya habari kwa
kutangaza na kuandika habari zilizofanywa na halmashauri hiyo.
Hafla ya kumkabidhi cheti cha shukrani  imefanyika leo katika ofisi za Chama Cha
Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC).
Dkt Mahera amesema Rais Dkt Magufuli alipowateua mwaka 2016
aliwataka wakajenge mahusiano mazuri na waandishi wa habari pamoja na jamii
ikiwemo viongozi wa dini na viongozi wa kimila.
“Nikiwa kwenye majukumu yangu ya kikazi niliteuliwa kuwa
Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi, nipende niwaahidi kwamba hata huku nilipo hivi
sasa nitaendeleza ushirikiano na waandishi wa habari katika kuendelea kujenga
mahusiano kama tulivyoelekezwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli,”alisema.
“Tumejitahidi sana kadiri ya uwezi wetu kujenga mahusiano na
kufanya kazi na waandishi wa habari  na
kwa kweli waandishi wa habari wa Arusha mlinipa ushirikiano wa kutosha,”.
Dkt Mahera pia amewashukuru waandishi wa habari wa vyombo
vya habari vya IPP MEDIA kwa kujitoa zaidi kwenye kuripoti taarifa za maendeleo
katika Halmashauri ya Arusha DC.
“Katika Halmashauri ya Arusha DC tulikuwa na kata 26 na
vijiji 68, maeneo yote haya tulifika na waandishi wa magazeti haya na stori zao
zilitoka, pia tulikutana na matatizo mbalimbali kama kunyeshewa na mvua na
kupigwa na jua lakini hatukata tama kwa kuwa yote tuliyafanya kwa maslahi ya
wananchi na taifa letu,”amesema.
Amesema agizo la Rais alilowaagiza wakurugenzi kulitekeleza
kuhusiana na kujenga mahusiano na jamii alilitoa Julai 12 mwaka 2016 baada ya kupokea
malalamiko mbalimbali wakati akiwa 
katika kampeni za uchaguzi mwaka 2015.
“Wakati nateuliwa ilinipatia wakati mgumu sana kwa kuwa
ilikuwa mara yangu ya kwanza kufanyakazi kwenye serikali za mitaa, rafiki zangu
walinikatisha tamaa lakini niliwaeleza wacha nikajaribu na kufanyakazi
nilitopewa heshima na Rais, na kwa kweli nilifanikisha,”amesema.
Amesema katika utumishi wake, amegundua kuwa katika Serikali
za mitaa kunahitaji  wasomi kwa sababu
ndio kiungo muhimu cha kupeleka mendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari
Mkoa wa Arusha (APC),  Claud Gwandu  alimpongeza kwa kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa
NEC na kumuahidi kuwa bado waandishi wataendelea  kutosha ushirikiano kwake katika kutekeleza
majukumu ya Serikali.
“Sisi kama waandishi wa habari na kwa niaba ya Chama, tunapenda
kukupongeza sana, katika utumishi wako ulijitoa bila kufanya ubaguzi ,
tutaendelea kukukumbuka kusaidia kupata kiwanja cha klabu, ulipokuwa mkurugenzi
tunashukuru sana,”alisema Mwenyekiti.