Mkurugenzi wa Jiji apiga marufuku walimu Arusha kuchangisha wanafunzi karatasi ‘Rim’

Egidia Vedasto, APC Media

Shule za Msingi na Sekondari za serikali na binafsi katika Jiji la Arusha zimeondokana na adha ya kuchangisha fedha kwa wanafunzi kwa ajili ya kununua karatasi za mitihani baada ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kutimiza ahadi ya kutoa pisi 2000 za (rim papers) .

Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi boksi hizo, amesema ni marufuku kuwachangisha fedha na kuwatuma karatasi, badala yake zitumike kwa shughuli hiyo na kuahidi zoezi hilo kuwa la muendelezo kwa wakati wote atakapokuwepo katika utendaji wake Jijini humo.

“Ninaamini Walimu wote hawa ni waelewa na watazingatia maelekezo kama yalivyotolewa juu ya rim hizi, zoezi hili limefanyika kwa muda muafaka ambapo Wanafunzi wanaelekea kufanya mitihani ya kumaliza mwaka” ameeleza Kayombo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule za Jiji la Arusha Peter Pantaleo amesema msaada huo utasaidia kumpungizia mzazi gharama za michango ya ununuzi wa karatasi za rim kwa ajili ya kufanyia mazoezi pamoja na mitihani mashuleni.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi (TAPSHA) Halmashauri ya Jiji la Arusha Peter Malealle amesema” tunamshukuru Mkurugenzi wetu ametekeleza ahadi yake aliyoahidi mwezi uliopita ili kufanya elimu yetu kuwa na tija, na tunaahidi kutendea kazi” .

Aidha mwakilishi wa walimu Yusta Njau amempongeza Mkurugenzi kwa hatua hiyo ya kuwapunguzia wazazi mzigo na kuwataka wanafunzi kuongeza jitihada katika masomo yao ili kuunga mkono juhudi za Mkurugenzi katika kuboresha sekta ya elimu.