Mo dewj: “niliwaambia walioniteka waniue”

Bilionea
kijana Afrika na mmiliki wa mojawapo ya klabu maarufu ya soka Afrika
mashariki Simba SC – Mohammed Dewji amezungumza kwa mara ya kwanza
kuhusu sakata lake la kutekwa nyara mwaka jana na namna alivyotishiwa
maisha yake nchini Tanzania.



Katika
mahojiano maalum na ya kipekee na BBC Swahili, Mo ameeleza kuwa kwa
kipindi kizima, alihisi kwamba kuna uwezekano mkubwa hatoweza kutoka
salama na kuwa mwisho wake wa maisha unakaribia.

“Saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi. Imani ndio kitu kikubwa kilichonisaidia katika kipindi kizima.”

Katika
kuikumbuka siku hiyo, Mo ameeleza: “Walinifunga macho, miguu na mikono
kwa siku tisa. Tulikuwa hatuongei sana, walikuwa sio watu wa hapa.

“Walikuwa wakinitisha na kuniweka bastola kwenye kichwa na kuniambia wataniua.” ameeleza mfanyabiashara huyo.

“Kufunga
mlango (wa gari) tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask
nyeupe – wamefunika uso, wakapiga bunduki juu mara mbili halafu
wameniwekea bunduki.”

Anasema
awali alidhani ni jaribio la kutaka kuibiwa gari, na hakuwa na budi
kufuata maagizo alipoambiwa alale chini kwenye sakafu.

“Kwenye sekunde sitini hivi, hao watu wamekuja wamenibeba na kuniweka ndani ya gari.”

Anasema
kilichofuata katika safari hiyo anayosema iliyokuwa ngumu, watekaji
wake walimvua nguo kwa kuhofia huenda ana kifaa cha kutambua anakokwenda
yaani tracker na kumfunga mikono na miguu na kwenye dakika 20
wakamfikisha katika nyumba.

“Niligundua kuwa lugha wanayotumia sio lugha ya Tanzania, ilikuwa ni geni.”

“Asubuhi
walikuwa wananifungua mikono wananifunga mbele, lakini usiku ndio
kulikuwa na mitihani walikuwa wananifunga nyuma. Na wakikufunga nyuma
maanake huwezi kulala, lazima ulale kulia au kushoto.”

Mo anasema alikuwa akitoa ushirikiano kwa kila alichotakiwa kufanya. Kikubwa anasema alikuwa akimuomba Mungu atoke salama.

Siku ya tisa anasema “walinisukuma pale Gymkhana na nikasikia gari limeondoka.”

Kwa muda wote alipewa tu kipande cha khanga aliyotumia kujifinika mpaka siku walipomuachilia ndiyo aliyotumia pia kujifunika.

Mo
Dewji alitekwa Oktoba 11 2018 na watu wasiojulikana alfajiri wakati
alipokuwa akielekea mazoezini alipofika katika hoteli moja ya kifahari
katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila
siku alfajiri kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

Siku tisa baadaye, Dewji alirejea nyumbani salama.

-BBC