Mpango bora wa ardhi utakavyouokoa ushoroba wa Kwakuchinja 

Miaka 18 baada ya kujiunga kwenye Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge wanakijiji katika vijiji vya Minjingu na Vilimavitatu katika kata ya Nkaiti wilayani Babati waliamua kwenda mahakamani kupinga sehemu ya maeneo yao kuingizwa kwenye jumuiya hiyo. 

Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge (JUHIBU) wanayotaka kujitoa wanavijiji hivyo, vilivyopo mkoani Manyara, ni miongoni mwa jumuiya bora nchini zinazopigiwa mfano kutokana na kufanya vizuri katika uhifadhi lakini pia kuwa msaada mkubwa wa kulinda ushoroba wa wanyamapori wa Kwakuchinja. 

Juhibu yenye ukubwa wa Kilometa za mraba 280, inayoundwa na vijiji  10 vya Kakoi, Olasiti, Magara, Maweni, Manyara, Sangaiwe, Mwada, Ngolei, Minjingu na Vilima Vitatu. Baadhi ya viongozi wa vijiji vya Vilimavitatu na Minjingu wanadai kuwa vijiji vyao vilitoa maeneo makubwa ya ardhi tofauti na vijiji vingine kwa ajili ya uhifadhi, kiasi cha kutaka mgao mkubwa wa mapato ama kujitoa kabisa kwenye jumuiya. 

Wataalam wa uhifadhi wanasema uwepo wa WMA ya Burunge iliyoanzishwa rasmi mwaka 2006 umesaidia kuokoa eneo kubwa la mapitio ya wanyamapori la Kwakuchinja  ambapo wanyamapori wamekuwa wakivuka upande mmoja kwenda upande mwingine kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na maeneo ya jirani. 

Hata hivyo tofauti na maeneo mengine yanayomilikiwa na kusimamiwa na vijiji, Burunge WMA inalindwa huku wananchi wakiruhusiwa kuchunga katika baadhi ya maeneo.

Migogoro ya ardhi baina ya vijiji hivyo na Serikali na matishio yoyote ya kujitoa kutoka kwenye vijiji wanachama yanahatarisha uhifadhi wa ushoroba wa Kwakuchinja ikiwemo uharibifu wa misitu na ujangili wa viumbepori vilivyopo.

Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge, Benson Mwaise anasema uhuru waliokuwa nao wanyamapori katika eneo hilo unatokana na ulinzi imara kutoka kwa askari wa jumuiya ya hifadhi ya Burunge waliofuvu mafunzo maalum ya kulinda wanyamapori.

Benson Mwaisa, Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi Wanyamapori Burunge

Tofauti na jumuiya nyingine  za hifadhi ya wanyamapori, JUHIBU imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na kuendelea kutunza bionuai wakiwemo wanyamapori na misitu huku idadi kubwa ya wanyamapori  ikiongezeka kwa kasi. 

Tishio la kijiji cha Minjingu kujitoa  kwenye jumuiya hiyo hasa baada ya kushinda kesi waliyofungua Mahakama Kuu na mahakama kuamuru eneo hilo lirejeshwe kwa wananchi  kunaelezwa na wataalamu wa uhifadhi kuwa tishio kwa Burunge WMA. Hii ni kwa sababu baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wameendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa ushoroba wa Kwakuchinja hasa katika maeneo ambayo hayajaingizwa kwenye jumuiya.

Kwa upande wa kijiji cha Vilimavitatu hususani wakazi wa kitongoji cha Maramboi kilichopo pembezoni mwa Hifadhi ya Ziwa Manyara,  Mahakama Kuu pia iliamuru wananchi hao warejeshewe ardhi yao kwa kuwa wamekuwa wakimiliki kisheria.

Wananchi wa kijiji cha Vilima vitatu wakiwa katika picha ya pamoja, wa kwanza kulia ni Udaghwenga Bayay kiongozi wa wananchi 17 waliofungua kesi dhidi ya Juhibu na kushinda

Udaghwenga Bayay, mmoja wa wananchi katika Kijiji cha Vilimavitatu waliofungua kesi hiyo, anasema wamefanikiwa kushinda kesi katika baraza la ardhi na nyumba dhidi ya Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori Burunge.  Katika rufaa ya madai namba 77 ya 2013 ambapo katika kesi ya msingi, Bi Udaghwenga akiongoza wananchi wenzake 17 katika Kitongoji cha Maramboi walikuwa wanadai kurejeshewa eneo lao ambalo wanadai lilichukuliwa kinyemela.

Mwenyekiti wa Kijiji cha vilimavitatu Abubakari Hatibu Msuya anahoji uhalali wa eneo la kijiji hicho kuchukuliwa na JUHIBU huku gawio ambalo wamekuwa wakilipata halionyeshi uhalisia wa eneo hilo.

‘Eneo kubwa, mapato kidogo’

“Sisi tulitenga eneo la hekta 4,600 kwa ajili ya utalii, lakini baadae wamefanya ujanja ujanja na kuchukua eneo lote la kijiji kuingiza kwenye jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Burunge na sasa tumeambiwa eneo la hekta 12,800 lote liko ndani ya JUHIBU, huku kijiji chote kikiwa na eneo la hekta 19,800,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Minjingu Samweli Melami anasema baada ya kushinda kesi dhidi ya JUHIBU, Serikali iliingilia kati kwa kukata rufaa na baadae kuiondoa kesi hiyo mahakamani kwa lengo la kufanya mazungumzo nje ya mahakama.

Mwenyekiti wa kijiji cha Minjingu Samweli Melami wa pili kutoka kulia akiwa na baadhi ya wajumbe wa Serikali ya Kijiji hicho pamoja na Afisa Mtendaji Salum Mbonde wa tatu kutoka kushoto

“Wananchi wanajiuliza haki yao iko wapi? Kwa nini eneo lao halirejeshwi? Huu ni mgogoro ambao hata sisi viongozi unatuweka njia panda, hatuaminiki kabisa na wananchi wetu, tunaonekana ni wasaliti,” anasema Mwenyekiti Samweli Melami huku akiongeza kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya Babati hadi sasa haijatatua mgogoro huo wa ardhi. 

Anasema mgogoro huo umekuwa ukififisha uhai wa ushoroba wa Kwakuchinja kwa kile wanachodai kuwa hawaoni tena umuhimu wa utunzaji wa eneo hilo la hifadhi lenye aina nyingi za wanyamapori sanjari na kuwa kivutio kikubwa kutokana na uwepo wa mandhari nzuri ya Ziwa Manyara na Ziwa Burunge.

Baadhi ya wananchi katika eneo hili wana hofu huenda siku zijazo wakaondolewa kabisa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya uhifadhi jambo ambalo mamlaka bado  hazijathibitisha uwepo wa mpango huo.

‘Uhifadhi ni kazi ya Mungu’

Uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge unakiri kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwa baadhi ya vijiji dhidi ya jumuiya hiyo lakini kwa sasa wamekuwa wakitoa elimu kuhusu faida za uhifadhi kuhakikisha wanamaliza migogoro hiyo.

“Uhifadhi ni sawa na kufanya kazi ya Mungu, inahitaji busara ya hali ya juu ili kuweza kumridhisha kila mtu, kuna baadhi ya watu katika vijiji hasa vijiji vya Vilimavitatu na Minjingu ambao hawajaridhika na maamuzi ya wengi kuhusu GN 2006 lakini pia tumegundua yote ni ubinafsi wa mtu mmoja mmoja,” anasema Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge, Benson Mwaise. 

Serikali inaeleza kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi iliyopo haikutakiwa kuwepo na kwamba siasa imechochea uwepo wake.

Siasa inachochea migogoro ya ardhi

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange ameiambia Arusha Press Club Blog kuwa Kijiji cha Minjingu hakina mgogoro na kudai kuwa kinachoendelea kijijini hapo ni siasa. 

“Huwezi kutaka kitu ambacho ni vigumu kukipata, pale hakuna mgogoro, wananchi wanataka haki ambayo sio rahisi kuipata,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange

Pamoja na uwepo wa migogoro hiyo ya ardhi,  vijiji  vinavyounda JUHIBU vimekuwa vikipata mapato kulingana na makusanyo ya uwekezaji wa utalii katika eneo hilo ambayo yamesaidia kuchochea maendeleo katika maeneo yao. 

Taarifa kutoka Juhibu zinabainisha kuwa mapato  ya uwekezaji katika jumuiya hiyo kwa mwaka 2021/2022 yaliongezeka na kuvuka lengo hadi Shilingi bilioni 1.2 tofauti na  makisio waliyojiwekea ya Shilingi bilioni 1.08.

Kutokana na mapato hayo, Mwaise anasema kwa mwaka huo, mgao wa jumla ulikuwa Shilingi Milioni 601.92 ambapo kila kijiji kilipata kiasi cha Shilingi Milioni 60.19 kwa idadi ya vijiji 10 vilivyopo kwenye jumuiya hiyo.

Hata hivyo takwimu zilizochapishwa na kubandikwa kwenye ubao katika ofisi hiyo zinaonyesha, mwaka 2017/18 mapato ya uwekezaji yalipanda na kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 2.07 ambapo kila kijiji kilipata gawio la Shilingi Milioni 103.6.

Chati inayoonyesha takwimu za Mapato yanayopatikana kutokana na uhifadhi kupitia eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge

Migogoro ya ardhi ni hatari kwa uhifadhi

Wataalamu wa uhifadhi wanaonya kwamba kuendelea kuwepo kwa migogoro inayotaka kuendeleza kukuza shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo la ushoroba ya Kwakuchinja hasa maeneo ya vijiji kunatishia mustakabali wa viumbepori kwa kuwa eneo hilo ni lango kuu la mazalia ya wanyamapori wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Ziwa Manyara.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya wanyamapori Tanzania (TAWA), Privatus Kasisi anasema kuendelea kuongezeka kwa wakazi katika ushoroba wa Kwakuchinja ni hatari kwa ekolojia ya eneo hilo ambayo imeunganisha maeneo mengi ya uhifadhi.

“Ekolojia ya ushoroba wa Kwakuchinja inaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Ziwa Manyara, inaenda hadi Mto wa Mbu Game Controlled Area, Lolkisale na Ranchi ya Manyara ambapo kote huko wanyama wamekuwa wakipita kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzaliana, maeneo mengine wanabeba mimba na mengine wanatumia kwa malisho,” anasema.

Anasema endapo ushoroba huo utaendelea kuachwa bila kuhifadhiwa ipasavyo ni wazi viumbe vingi vitapotea ikiwemo baadhi ya aina za wanyamapori lakini pia wananchi watakosa huduma za msingi kutokana na mapato ambayo wamekuwa wakiyapata hivi sasa kupitia ushirika wa jumuiya za hifadhi ikiwemo Burunge WMA.

Kuhusu madai ya baadhi ya vijiji kutishia kujiondoa kwenye Jumuiya ya Juhibu kutokana na kulipwa fedha ambazo hazilingani na ukubwa wa maeneo waliyoyatoa, Kasisi anasema: “kabla ya kukubali kuingia kwenye huu ushirika waliweka makubaliano, hivyo kinachopaswa kufanywa hivi sasa ni vile vijiji ambavyo vinaona havitendewi haki viwasilishe hoja kwenye mamlaka husika  na kufanya mazungumzo kwa ajili ya maridhiano.”

Mpango bora wa ardhi utaokoa ushoroba

Wadau wa  uhifadhi wanasema ili kuondoa sintofahamu na uhasama uliopo kati ya Serikali na wananchi  Serikali inapaswa kuweka wazi mchakato mzima wa upangaji wa matumizi bora ya ardhi na kuainisha wazi mashamba na maeneo ya machungio ili wananchi waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi.  

Mdau wa uhifadhi na mwekezaji katika eneo la Burunge WMA, Willy Chambulo anasema ili kuondoa migogoro iliyopo ni lazima Serikali ikae na wananchi wa vijiji vyenye migogoro na kupanga upya matumizi bora ya ardhi huku ikiainisha maeneo ya uhifadhi, mashamba kwa ajili ya kilimo na ufugaji ili kujiendeleza kiuchumi.

Hata hivyo, anasema mgawanyo wa rasilimali fedha inayopatikana kutokana na makusanyo ya uwekezaji  katika eneo hilo ni suala ambalo linapaswa kufanyiwa majadiliano kwa kuwa kuna vijiji vimetoa maeneo makubwa kuingiza kwenye JUHIBU lakini mapato wanayopata yamekuwa sawa kwa kila kijiji.

Serikali kuongoa shoroba 20 za kipaumbele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki alilieleza Bunge wakati akiwasilisha  hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2024/2025 kuwa hadi kufikia Aprili 2024, Serikali ilikuwa katika hatua mbalimbali katika uongoaji wa shoroba nane kati ya 20 za kipaumbele.

Shoroba zinazoendelea kuongolewa  ambazo ni kati ya 20 za kipaumbele zilizoko katika hatua mbalimbai ni Udzungwa – Nyerere, Katavi – Mahale, Ruaha – Katavi, Rungwa – Ruaha, Tarangire – Manyara (Kwakuchinja), Ngorongoro – Manyara (Upper Kitete) na Lake Manyara – Ngorongoro (Yaeda Chini).

Tanzania ina shoroba 61 na ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi ukiwemo mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Watu wa Marekani wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya kuongoa shoroba nchini ukiwemo ushoroba wa Kwakuchinja ili kulinda bioanuai katika maeneo hayo.

“Kutokana na baadhi ya vijiji vinavyopakana na maeneo yaliyohifadhiwa kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi wizara kupitia TANAPA imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 74 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa za Serengeti ambavyo ni 37, Ziwa Manyara (25) na Tarangire vijiji 12. Utekelezaji wa mipango hii utasaidia kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori,” alisema Waziri Kariuki.

Ripoti hii maalum ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili. 

************************************************************************************