Mwenyekiti auawa akitatua mgogoro wa ardhi kijijini

Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira
wilayani Kiteto mkoani Manyara, Engerusi Mikonde (59), ameuawa katika
shamba moja akiwa kwenye harakati za kutatua mgogoro wa ardhi ambao
unadaiwa kuwa ungeleta madhara kati ya wakulima hao.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Augostino
Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema uchunguzi unaendelea
na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya
Kiteto.

Mmoja ya wakazi walioshuhudia tukio hilo
Daiomoni Nzungu, amesema Mikonde akiwa na kamati ya mazingira kutafuta
ufumbuzi wa mgogoro wa wakulima Kijijini hapo, alishambuliwa kwa marungu
na mapanga hadi alipokutwa na umauti.

Baadhi ya wananchi wamelitaka jeshi la
polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo wakisema kuwa suluhu
ya sakata hilo ni kupatikana kwa taarifa ya kina ili sheria ifuate
mkondo wake kwa waliohusika.

Migogoro mingi ya wakulima na wafugaji
wilayani Kiteto huanza kipindi ambacho wakulima wanaandaa mashamba huku
wafugaji wakihitaji maeneo kwaajili ya shughuli za kufugia mifugo yao.
CHANZO – MTANZANIA