Naibu waziri wa afya dkt. ndugulile ataka taarifa utoaji wa dawa hospitali ya rufaa iringa.

Na Mwandishi Wetu Iringa

Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt.
Faustine Ndugulile amemuagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt.
Atupele Mwandiga kuhakikisha anapata taarifa ya utoaji wa dawa katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.

Agizo
hilo limekuja mara baada ya ziara ya yake mkoani humo alipotembelea
hospitali hiyo kujionea utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na
kushuhudia mmoja wa mama aliyejifungua Hospitalini hapo kupewa dawa mara
moja badala ya mara tatu kama iilivyoandikwa na Daktari.

Dkt.
Ndugulile amesema kuwa amekasirishwa na utendaji kazi wa manesi katika
wodi ya Mama na Mtoto kwa kutozingatia utoaji huduma hasa kuhakikisha
wazazi na watoto wanapewa dawa kwa wakati zinazotakiwa na kwa idadi
sahihi.

Ameongeza
kuwa lengo la mgonjwa kupewa huduma ni kuhakikisha anapona na sio
kufanya aendelee kupata tabu na shida hivyo Serikali ya Awamu ya Tano
imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha Sekta ya Afya inaboreshwa
nchini.

“Haiwezekani
mgonjwa kanunua dawa zake kwa fedha zake lakini bado hata hamzingatii
kumpatia dawa mnategemea ataponaje” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha
Dkt. Ndugulile ameutaka uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa
kuhakikisha wanaratibu utoaji wa huduma hospitalini hapo ili kuepukana
na malalamiko ya wagonjwa na kupoteza imani ya wananchi kwa Hospitali
hiyo.

“Tukiendelea
hivi tutaondoa imani kwa wananchi wetu katika utoaji wa huduma za afya
sisi tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi na sio kuwapa kero wananchi”
alisema Dkt. Ndugulile.

Kwa
upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga
amemuahikikishia Naibu Waziri Dkt. Ndugulile kusimamia utoaji huduma
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kusimamia vilivyo ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili.

Ameongeza
kuwa Serikali ya Awamu ya tano imetoa kiasi cha Billioni 7 kwa ajili ya
ujenzi wa Hospitali za Wilaya na maboresho katika Zahanati na vituo vya
Afya mkoani humo katika kuhakikisha inaboresha Sekta ya Afya hivyo
watasimamia Sekta hiyo kikamilifu.

“Mhe.
Naibu Waziri tutahakikisha hatutopoteza imani ya wananchi katika utoaji
huduma za afya na tutatendea haki rasimali fedha tulizopewa na Serikali
katika kuboresha Sekta ya Afya Mkoani kwetu” alisema Dkt. Atupele

Wakati
huo huo Dkt. Ndugulile ametembelea na kujionea utendaji kazi utoaji wa
huduma kwa wananchi katika Ofisi ya Bima ya Afya (NHIF), Kampeni ya
masuala ya Lishe, Kiwanda cha Ruaha Milling na ujenzi wa Hospitali ya
Wilaya ya Kilolo.

Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt.
Faustine Ndugulile yuko katika ziara ya siku mbili mkoani Iringa
kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii mkoani humo.