Naibu waziri wa maliasili na utalii, mhe.kanyasu aagiza ngombe 179 zilizokuwa zimekamatwa ziachiwe

Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameiagiza
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) kuiachia na
kuirudisha mifugo zikiwemo jumla ya ng’ombe 179 zilizokuwa zimekamatwa
ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero ambayo ni Mali ya Mathayo Marao, 
Mwananchi wa Kijiji cha Kimotorok kilichopo ndani ya Pori hilo katika
wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa makubaliano ya kutoingiza tena
mifugo hiyo.


Uamuzi
huo umekuja kufuatia utata uliopo eneo ilipokamatiwa mifugo hiyo kwa
vile  Kijiji hicho cha Kimotorok ni miongoni mwa Vijiji na Vitongoji 366
vilivyo ndani Hifadhi na vinavyosubilia maamuzi ya Rais wa Tanzania,
Mhe.John PombeMagufuli na moja kati ya maagizo aliyoyatoa  kwamba 
wananchi wa Vijiji hivyo   wasibugudhiwe hadi pale maamuzi ya mwisho
yatakapotolewa.
Kwa
mujibu wa Wahifadhi, Mifugo hiyo iliyokamatwa mwishoni mwa mwaka jana
inadaiwa kukutwa mita 450 ndani ya Pori hilo huku Wananchi wakidai kuwa
Mifugo hiyo ilikutwa nje ya mita 450 kutoka kwenye mpaka mahali ambako
wamekuwa wakiishi huku wakisubiri kauli ya mwisho ya Mhe.Rais.

 Mvutano
huo baina  ya Wahifadhi na Wananchi umempekelea Mhe.Kanyasu kutumia
busara na  kufikia uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa Kijiji hicho kipo
ndani ya Hifadhi.

Kutokana
na majadiliano ya pande hizo mbili, Naibu Waziri huyo amelazimika  
kutoa uamuzi huo wa kuachia  mifugo hiyo kwa makubaliano ya Wananchi wa
Kijiji hicho  kuheshimu sheria za Uhifadhi kwa  kutoingiza mifugo ndani
ya Hifadhi  hadi pale maamuzi ya mwisho yatakapotolewa na Rais Magufuli.

Akizungumza
jana katika mkutano huo uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok, Naibu
Waziri Mhe.Kanyasu amesema uamuzi huo umefanyika kwa busara kwa vile
mifugo hiyo ilibidi ipelekwe mahakamani.
Amesema
kitendo cha kuacha kupeleka kesi hiyo mahakamani kinasaidia kupunguza
idadi kubwa ya mifugo kufa ambapo hadi sasa zaidi ya ndama kumi
wameshakufa.

Kufuatia
hali hiyo, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi hao kuacha kutumia vibaya
kauli ya Rais Magufuli kwa kuanza kuvamia maeneo mapya ya Hifadhi kwa
kisingizio cha kauli hiyo ilhali wanatakiwa kubaki na mifugo yao mahali
walipo.
Amefafanua
kuwa kulikuwa na uwezekano wa kupeleka mifugo hiyo mahakamani ila
kutokana na Wananchi hao kuomba maridhiano kwa kutambua kuwa wametenda
kosa imepelekea mifugo hiyo kuachia.

Katika
hatua nyingine, Mhe Kanyasu amesema Serikali haipendi kutaifisha mifugo
inayokamatwa Hifadhini kama sheria inavyoelekeza kwa vile wananchi
wengi wamejikuta kwenye umaskini wa hali ya juu, Hivyo amewataka
wananchi hao kuacha tabia ya kuingiza mifugo hifadhini kwa vile
watafrisiwa.


Serikali inafurahi kuona Wafugaji wananeemeka kupitia mifugo yao huku
uhifadhi ukiendelea kwa maslahi mapana ya Taifa” alisisitiza Kanyasu

Aidha,
Mhe.Kanyasu ametoa onyo kwa Wananchi wanaovamia Wahifadhi wakiwa
wanatekeleza majukumu yao na kuahidi kuwa Serikali haitamvumilia
Mwananchi yeyote atakayethubutu kutumia mabavu dhidi ya Wahifadhi.


Tukikubaini ni miongoni mwa Mwanakijiji uliyejitokeza ukiwa umeshika
mkuki au unapiga mwano kwa nia ya kuwahamasisha wenzako kwa ajili ya
kuwadhuru Wahifadhi, Tutakushughulikia ipasavyo” Alisisitiza

Kwa upande wake Mbunge wa Simanjiro, Mhe. James Millya amewataka wananchi waache tabia ya kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi.

Pia
amelaani vikali vitendo vya baadhi ya  wananchi wanaohamasisha ghasia
kwa Wahifadhi na kuahidi kuwa yeye hatakuwa tayari kumsaidia mwananchi
yeyote atakayekamatwa kwa kutenda kosa hilo kwa vile Wahifadhi hao
wanafanya kazi za kulinda Hifadhi hizo kwa niaba ya Watanzania wote.
Kufuatia
hali hiyo, Mhe.Millya amewataka Wazee wa mila ‘Olaibon’ kutumia nafasi
hiyo kwa kuitaka jamii yao kufuata sheria za Uhifadhi kwa kuheshimu
Sheria zilizopo zinazokataza kulisha mifugo ndani ya Hifadhi

Akizungumza
kwenye mkutano huo, Mhe.Millya amewataka Wananchi hao kila mmoja awe
Mlinzi wa mwenzake kwa kuimarisha ujirani mwema kati ya Wananchi na
Wahifadhi badala ya kuendekeza uhasama kwa kuingiza mifugo ndani ya
Hifadhi.

Awali,
Joseph Olematwaa ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho alisema uamuzi wa
kuachia mifugo utarudisha mahusiano mema kati ya Wahifadhi wa Pori hilo
na Wananchi na kuahidi kuwa hawataingiza tena mifugo ndani ya Hifadhi.