Nmb yashauriwa kutumia fursa za kibiashara sekta ya madini


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akisisitiza jambo wakati wa kikao baina yake na Ujumbe kutoka Benki ya NMB pamoja na Wataalam kutoka Wizara ya Madini.


Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Serikali ya Benki ya NMB, Vicky Bishubo, akieleza jambo wakati wa kikao baina ya Benki hiyo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini. Wengine wanaofuatilia ni Watalaam kutoka Benki hiyo.


Wataalam kutoka Benki ya NMB wakifurahia jambo wakati wa kikao baina yao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msajil (hayupo pichani)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya NMB pamoja na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Athony tarimo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini prof. Simon Msanjila akiongoza kikao baina ya Ujumbe wa Benki ya NMB na Wizara ya Madini.


Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Madini Anthony Tarimo akifuatilia sambamba na Mtaalam kutoka benki ya NMB Josephine Kulwa wakari wa kikao baina katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila na Ujumbe kutoka Benki ya NMB.




Na Asteria Muhozya, Dodoma



Benki ya NMB imeshauriwa kutumia fursa za Kibiashara zilizopo katika Sekta ya Madini zikiwalenga Wachimbaji Wadogo na wa Kati wanaofanya shughuli hizo katika sekta husika ikiwemo

kujifunza namna biashara ya Madini inavyofanyika.



Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila wakati wa kikao baina yake na Ujumbe wa Wataalam kutoka Benki hiyo ulioongozwa na Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Serikali ya Benki hiyo, Vicky Bishubo. Kikao hicho kimefanyika Novemba 25, 2019, jijini Dodoma.



Aidha, kauli ya Katibu Mkuu kwa benki hiyo inafuatia juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini zinazolenga katika kuwapatia elimu Wachimbaji ikiwemo za kutunza kumbukumbu za uzalishaji, kufanya tafiti ili kujua kiasi cha mashapo kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), hayo yote yakilenga katika kuwawezesha wachimbaji hao kukopesheka na Taasisi za Fedha.



Pia, Prof. Msanjila ameitaka benki hiyo kutumia fursa zilizopo katika masoko ya Madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini ili kurahisisha biashara ya Madini na kutolea mfano wa Soko la Madini Arusha kwamba benki hiyo haina huduma katika soko hilo huku biashara ya Madini sokoni hapo ikifanyika kwa kiasi kikubwa.



Aidha, Prof. Msanjila ameitoa wasiwasi benki hiyo kuwa, hivi sasa biashara za Madini zinafanyika katika mfumo ulio wazi tofauti na ilivyokuwa awali na kuongeza kwamba, “kuna biashara nyingi
kwenye sekta ya madini. Niwaambie hivi karibuni Serikali ya Qatar itaanza kununua dhahabu moja kwa moja kutoka Geita.”



Katika hatua nyingine, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 35(j) ya Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015-2020 kuhusu Kusimamia na kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa, Prof. Msanjila ameishauri benki hiyo kuangalia namna ya kufanya biashara katika tasnia ya ukataji wa madini, akieleza kwamba, ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele na serikali ya kuhakikisha madini yanaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.



“Sekta ya madini haijatumiwa vizuri na mabenki ninawakaribisha kwenye sekta hii . Pale Arusha ndo mji pekee wa Ukataji Madini ya Vito. Mwende mkaliangalie hili,” amesisitiza Prof. Msanjila.



Naye, Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Serikali ya Benki hiyo, Vicky Bishubo amemshukuru Prof. Msanjila kwa kueleza fursa zilizopo katika sekta husika na kueleza kwamba, benki hiyo imeyachukua kwa uzito mkubwa yote yaliyoelezwa na iko tayari kuyafanyia kazi.

“Tumejifunza namna sekta ya Madini inavyofanya kazi kuna uwezekano wa sisi kuandaa mfumo wa kuwasaidia wachimbaji wadogo,” ameeleza Bishubo