Rais magufuli : kususia uchaguzi nayo ni demokrasia… aipongeza ccm ushindi uchaguzi serikali za mitaa

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli amesema kitendo cha kususia uchaguzi wa
serikali za mitaa huku akikisitiza kuwa maendeleo hayana chama na kwamba
Watanzania wanatakiwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa. 

Rais Magufuli ameyasema hayo leo
Jumatano Novemba 27,2019 wakati akizungumza na wananchi wa Isaka
wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Rais Magufuli amekipongeza Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwa ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa
uliofanyika Novemba 24,2019.
“Ninapenda kuwashukuru sana ndugu
zangu wa Isaka mmemaliza chaguzi, Nimeambiwa Chama Cha Mapinduzi
kimepasua vizuri. Hongereni sana,maendeleo ndugu zangu hayana chama na
demokrasia hata kujitoa nayo ni demokrasia,kususia uchaguzi nayo ni
demokrasia”,
amesema Rais Magufuli. 

“Kwa hiyo nawapongeza kwa ushindi
mkubwa mlioupata chama cha mapinduzi lakini maendeleo hayana chama ni
lazima tushikamane wote kujenga taifa letu,tunachohitaji ni
maendeleo,ukileta maji,wote watakunywa,uwe CCM, uwe CHADEMA,ukileta
bandari hapa kila mmoja atafanya biashara”,
ameongeza Rais Magufuli. 

“Naomba Watanzania tutangulize mbele maslahi ya taifa letu,tuwe wamoja,tujenge Tanzania yetu”,amesema Rais Magufuli.


Hii ni kauli ya kwanza kutolewa
na Rais Magufuli tangu baadhi ya vyama vya upinzani kumwomba kuingilia
kati madai yao ya wagombea wao kutokutendewa haki wakati wa shughuli ya
uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uchaguzi huo uliofanyika
Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019.
 Baadhi ya Vyama vya Upinzani nchini Tanzania vilisusia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa madai ya kutokutendewa
haki wakati wa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea
uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita Novemba 24, 2019.