Rc mnyeti : wananchi dongobesh wapokeeni wafanyakazi wa halmashauri ya mbulu

Na Mwandishi Wetu, Manyara
WANANCHI wa kata ya Dongobesh wilaya ya
Mbulu mkoani Manyara wametakiwa kuwapokea na kuwakaribisha wafanyakazi
wa halmashauri hiyo ambapo wanatarajia kuhamishia makao makuu ya
halmashauri hiyo ndani ya wiki hii.


Kauli hiyo imetolewa juzi na mkuu wa
mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alipotembelea na kukagua jengo jipya la
halmashauri ya wilaya ya Mbulu linalojengwa kwenye kata hiyo. 

Mnyeti alisema  ujio wa watumishi hao wa
halmashauri kwenye kata ya Dongobesh utaleta mabadiliko ya haraka
lakini pia mji utachangamka na maendeleo yataonekana kwa haraka zaidi. 

“Sasa nikuombe Mwenyekiti 
uwahamasishe wananchi wa Dongobesh wawapokea watumishi kwa sababu
tunaambiwa hapa kuna Ka Ukoo fulani ambako ndiko kana dominate kila kitu
sasa kama mkifanya hivyo shauri yenu. 

“Lakini mkitaka maendeleo muwapokee
watumishi, msiwafanye watumishi usiku wamelala wanaamka  wanajikuta wapo
barabarani maana tunasikia kwamba hapa Dongobesh ni wataalamu sana wa
sekta hiyo. 

“Niwaombe muwapokee watumishi na
kuwafanya kama watoto wenu, sio tukileta hapa watumishi halafu mkawa
mnawafanyia mambo ya namna hiyo tutawaondoa, tutajenga nyumba za
halmashauri maeneo mengine watakuwa wanakuja kufanya kazi wanaondoka”,
Alieleza Mnyeti. 

Hata hivyo Mnyeti alishauri kwamba pindi
watumishi wa halmashauri hiyo watakapohamia kwenye eneo hilo uitishwe
mkutano wa wazee wa kimila wawapokee na kuwapa ulinzi wa kimila
asidhurike mtu hata mmoja. 

Pamoja na hayo Mnyeti alipongeza kazi ya
ujenzi unaoendelea kwenye jengo la halmashauri hiyo ambalo linajengwa
na kampuni ya kijeshi ya Mzinga ambapo alidai kuwa fedha iliyotolewa
inaendana na kazi inayofanyika. 

“Ingelikuwa tumetoa pesa halafu
hakuna kinachofanyika tungesikitika sana, mwanzoni nilipita hapa
nilimkuta mzee mmoja  tu na hapakuwa na mtu mwingine, nilisikitika sana 
 kwa sababu Mzinga tunaowaamini ni makampuni ya kijeshi ambayo
tunaamini kwamba kazi zao zinakwenda kijeshi tulitoa mawazo yetu, 
tulitoa ushauri na mmetekeleza tunawapongeza sana. 

“Sasa mlichonishawishi ni kitu kimoja
tu kikubwa kwenda kuwatafutia pesa ili ije pesa nyingine muweze
kuendelea na ujenzi huu na kwa spidi hii kwa kweli mmetufurahisha kwani
hakuna kitu kibaya kama kuletewa pesa halafu miradi inakuwa haiendi”,
alisema.  

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa
halmashauri ya wilaya ya Mbulu Joseph Mandoo alipongeza kazi kubwa
inayofanywa na Rais Magufuli kwa kusimamia fedha za watanzania kutokana
na huko nyuma kutokuwa na historia nzuri. 

“Sisi wana Mbulu niseme ametupendelea
sana kwa sababu ametupa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye shule za
sekondari na msingi lakini kubwa zaidi ni kutuletea fedha bilioni mbili
na milioni Mia tano kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri ya
wilaya katika mji wa Dongobesh lakini pia ametuletea fedha zaidi ya
bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya”,
alieleza Mandoo