Serikali inaandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi urithi wa ukombozi wa afrika

Malunde       Tuesday, December 3, 2019

Na Eleuteri Mangi, Kongwa
Serikali
inaendelea kubainisha maeneo yaliyotumiwa na wapingania uhuru wa nchi
za Kusini mwa Afrika ambayo yanasimamiwa kupitia Programu ya Urithi wa
Ukombozi wa Afrika iliyopo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo.

 

Akiwa
katika ziara ya kikazi wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati
akitembelea maeneo ya historia ya Ukombozi wa Afrika, Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa Serikali kupitia wizara
hiyo inaandaa sheria ya kulinda na kuhifadhi urithi wa ukombozi wa
Afrika unaopatikana nchini.
“Lengo
kubwa ni kuhakikisha maeneo haya yanalindwa kisheria ili yaweze
kutumika kama vivutio vya utalii wa kiutamaduni pamoja na utalii wa
kihistoria kwa sababu huu ni urithi muhimu wa historia nzuri ya nchi
yetu, haya ni maeneo yaliyotumika kusaidia ukombozi wa Nchi za Kusini
mwa Afrika” alisema Naibu Waziri Shonza.
  
Katika
kutekeleza Programu ya Uhifadhi na Uendelezaji wa historia ya Ukombozi
wa Afrika, Wizara inaendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo,
ukarabati wa jengo lililokuwa la Kamati ya Ukombozi ya iliyokuwa Umoja
wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Kazi
nyingine ambazo Serikali imekamilisha ni uandaaji wa tovuti ya
Programu, ubainishaji wa maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za
ukombozi, utambuzi wa nyaraka na vitu mbalimbali vinavyohusiana na
harakati hizo pamoja na kufanya mahojiano na watu walioshiriki au
kushuhudia harakati za ukombozi wa Afrika ambayo yamehifadhiwa kwa njia
ya kidigitali.
Mji
wa Kongwa kihistoria ni kitovu cha harakati za Ukombozi wa Afrika kwani
harakati zote za mapambano ya kutafuta uhuru zilianzia Kongwa na
baadaye zikaendelea katika maeneo mengine nchini kama sehemu ya kupanua
wigo wa harakati hizo na huduma kwa Wapigania Uhuru.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Deogratius Ndejembi amesema kuwa Kongwa
ni eneo kongwe lililotumiwa na Wapigania uhuru kutoka vyama mbalimbali
vya Ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika. 
Aidha,
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa eneo hilo lilitumika kwa ajili ya
mafunzo kwa wapigania uhuru ambapo kwa sasa lina vielelezo muhimu vya
kihistoria vilivyopo katika eneo hilo yakiwemo maeneo ya Handaki
alilokuwa akilitumia Samora Mashel, nyumba za Makazi kwa wapigania
uhuru, majengo ya shule ya sekondari Kongwa, eneo la Mafunzo ya kijeshi,
kiwanja cha ndege na makaburi ya wapigania uhuru. 
Maeneo
mengine ya kihistoria ni makaburi ya mashujaa wa harakati za ukombozi
ambayo jumla yake ni 11; makaburi matano ya wapigania uhuru kutoka
Msumbiji, makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Afrika Kusini na
makaburi matatu ya wapigania uhuru kutoka Namibia.

Naibu
Waziri Shonza yupo katika ziara ya kikazi kutembelea maeneo ya ya
historia ya ukombozi wa Afrika katika mikoa ya Dodoma wilaya ya Kongwa,
Morogoro wilaya Kilosa, Manispaa ya Morogoro pamoja na Mkoa wa Pwani
wilaya za Chalinze na Bagamoyo