Serikali kuanzisha vituo vya malezi ya watoto nchi nzima

Na Mwandishi Wetu
Serikali imeanza mpango wa kuwa na vituo vya malezi kwa watoto nchini
nzima ili kuhakikisha wanajamii wanayapa kipaumbele malezi na makuzi kwa
watoto ili kuhakikisha kunakuwa na taifa madhubuti.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema hayo leo
jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Semina ya Mafunzo ya Elimu ya
Malezi, maendeleo na makuzi kwa wakufunzi kutoka vyuo vya Maendeleo ya
Wananchi.

Dkt. Jingu amesema kuwa vituo hivyo vitaratibiwa na Serikali ila
vitaendeshwa na kusimamiwa na wananchi katika maeneo yao na mpaka sasa
kuna zaidi ya vituo 1500 nchi nzima na vingine vinaendelea kuanzishwa.

Ameongeza kuwa malezi ni msingi mkubwa katika kuhakikisha tunapata
kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uzalendo katika kizazi
itakayosaidia kujenga taifa bora.

“Mafunzo haya ni muhimu na mmeamua suala sahihi, watoto wanahitaji
malezi ya karibu na sio malezi tu bali wapate malezi sahihi” alisema
Dkt. Jingu

Dkt. Jingu pia amewataka washiriki wanatumia stadi hiyo kuisaidia jamii
na nchi kuweza kuwa na muelekeo mzuri kwa kuwa na vijana wazalendo
wawajibikaji kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Noel Mbonde amesema kuwa Wizara ya Elimu
itahakikisha inashirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha  Elimu ya
Malezi, maendeleo na makuzi kwa watoto inatekelezwa.

Ameongeza kuwa Wizara ya Elimu imehakikisha kila Chuo cha Maendeleo ya
wananchi kinakuwa na kituo cha kulea watoto ili kuhakikisha inawasaidia
watoto.

Naye Mwakilishi wa washiriki ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya
Jamii Mbinga Bw. Lotty Mwang’onda amesema kuwa mafunzo waliyoyapata
yatawasaidia kuleta mabadiliko hasa katika jamii inayowazunguka katika
vyuo vyao ili kuhakikisha malezi, maendeleo na makuzi yanazingatiwa
katika ukuaji wa mtoto.

Ameongeza kuwa wao kama washiriki wameshukuru kwa uzoefu na kama
wataalam wa wanaofanya kazi na jamii watashirikiana na jamii kuhakikisha
elimu walioyoipata inawafikia jamii inayowazunguka.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Karibu Tanzania KTO Bw. Aidan
Mchawa ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa ushirikiano wao na
asasi za kiraia katika kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi na
kuhakikisha program ya Malezi, maendeleo na makuzi ya awali ya mtoto
inarudisha misingi ya malezi ya mtoto hasa wa kitanzania.

Naye mshiriki Bi. Felister Nanguka ameishukuru Serikali kwa kuwezesha
upatikanaji wa elimu ya mafunzo ya Malezi, maendeleo na makuzi katika
jamii hasa vijijini na kuahidi kufanya kazi hiyo kwa nguvu zao kwa
kukaza msuli ili kuhakikisha watoto wanapata malezi stahili.

Shirika la Karibu Tanzania KOT limeandaa mafunzo kwa wakufunzi kutoka
vyuo kumi vya Maendeleo ya Wananchi nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo
kuhusu malezi, maendeleo na makuzi ya awali ili wakaitoe elimu hiyo kwa
jamii inayowazunguka.