Serikali kuwawajibisha maafisa kilimo watakaoshindwa kusimamia kilimo

Na Amiri kilagalila-Njombe

Serikali
nchini imesema maafisa kilimo wanatakiwa kumsimamia na kumpa maelekezo
mkulima ili kulima kilimo chenye tija,kutokana na wakulima wengi kutumia
ardhi kubwa lakini matokeo yanayopatikana yamekuwa hayana tija.

Waziri
wa kilimo,ushirika na umwagiliaji Mh.Japhet Hasunga amesema serikali
itawawajibisha maafisa kilimo endapo itabainika wakulima wanatumia ardhi
kubwa katika kilimo bila ya kutumia maarifa.

Waziri
Japhet Hasunga ameyasema hayo wilayani Njombe mkoani Njombe wakati
akikagua mradi umwagiliaji wa kikundi cha Twilumba uliopo kijiji cha
Itipingi kata ya Igongolo wilayani humo.

“Nataka
niwapongeze mliposema mmeongeza tija,mmeniambia mmeongeza kwa mfano
nyanya mlikuwa mnapata tani 12 sasa zimefika 30,lakini pamoja na
mafanikio hayo nilikopita mashamba yale hayajanivutia kwasababu naona
mnavyolima mmeweka hatua kubwa kwa hiyo mnatumia eneo kubwa mavuno
kidogo”alisema waziri Hasunga

Kutokana
na hilo Waziri hasunga akatumia nafasi hiyo kuwaagiza maafisa kilimo
nchini kuwasimamia na kuwaelekeza wakulima ili kubadilisha kilimo.

“Maafisa
kilimo hatuko kumshauri mkulima kwa sasa tunatakiwa kumpa maelekezo na
kumsimamia,maana sasa hivi nikienda mahali nikakuta wananchi wamelima
vibaya hawajatumia maarifa,wanalima kilimo cha hovyo,wanatumia ardhi
kubwa tija kidogo wanaotakiwa kuwajibika ni maafisa kilimo kwasababu wao
ndio wapo kwenye hayo maeneo”alisema Hasunga

Awali
akisoma taarifa ya mradi wa umwagiliaji wa twilumba muweka hazina wa
mradi huo Amasinze Kadwame,amesema mradi huo uliojengwa kwa ghalama ya
milioni 400 ukiwa na urefu wa mita 1725 una idadi ya wanachama 74 hivyo
licha ya upatikanaji wa faida kubwa kutokana na mradi huo wanaiomba
serikali kuongeza mradi huo ili kuongeza idadi ya wakulima na mashamba
kutokana na uwingi wa maji katika mradi.

“Sisi
wakulima kulingana na namna mradi ulivyosanifiwa maji ni mengi tuomba
kuongezewa mradi ili kuongeza idadi ya wakulima na mashamba hadi kufika
ekari 400 zilizofanikiwa tuongeze uzalishaji na mapato ya halmashauri
kupitia ushuru kama serikali inavyohimiza kwa mazao yanayolimwa”alisema
Amasinze Kadwame

Nickson
Kibiki na Joyce Mbembati ni miongoni mwa wakulima wanaotumia mradi
huo,wanasema mradi huo umewawezesha kuongeza uzalishaji ukilinganisha na
awali hatua iliyowawezesha wananchi kukuza uchumi wa vipato vyao pamoja
na kuwapeleka watoto shule.