Serikali ya awamu ya tano kuendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia takwimu

  


Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro Bw. Adam Mgoi akizungumza Wilayani Bahi mkoani Dodoma Oktoba 
kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani   Jafo wakati wa hafla ya uzinduzi na
usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya
Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.




Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa  akieleza faida za
kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa kutumia mfumo wa kidigitali kwa
ajili ya Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022
wakati wa hafla ya uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo 
hayo iliyofanyika Wilayani Bahi mkoani Dodoma.



Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe.
Mwanahamis  Munkunda akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi na
usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya
Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.



Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Bw. Wilfred Ochan akieleza
kuhusu mikakati ya Shirika hilo kuunga mkono  mikakati ya Serikali
kufanikisha Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.



Mwakilishi  kutoka Benki ya Dunia
Bi. Elizabeth Talbert akizugumzia umuhimu wa sense na zoezi ya kutenga
maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi
inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.



Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro Bw. Adam  Mgoi akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa
Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo
alimuwakilisha  Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kuzindua taarifa ya
Wilayani Bahi mkoani Dodoma baada ya kukamilika kwa zoezi za kutenga
maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya sensa ya watu na makazi ya mwaka
2022 ,hafla hiyo iliyofanyika Oktoba 17, 2019 wilayani humo.


………………


Na Mwandishi Wetu- Bahi


Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia takwimu
zinazokusanywa ili kuwezesha kupangwa kwa mipango ya maendeleo
inayoendana na mahitaji ya wananchi katika huduma za jamii.


Akizungumza Oktoba 17, 2019 huko
Bahi mkoani Dodoma wakati wa uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya
kutenga maeneo ya kuhesabia watu ya Wilaya ya Bahi, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo alisema
kuwa taarifa zinazotokana na takwimu zitasaidia katika upangaji wa
mipango unaoendana na mahitaji ya wakati.


Katika hotuba yake iliyosomwa kwa
niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoi, Waziri Jafo
alieleza ili kutekeleza dhamira ya serikali ya kuwatumikia vyema
wananchi ni lazima kufahamu idadi ya wananchi wake, hali zao za
kiuchumi, mahali walipo, elimu yao, afya zao na mahitaji yao ya msingi.


Aliueleza mkutano huo kuwa Takwimu
zinazokusanywa wakati wa Sensa ni nyenzo muhimu kwa utayarishaji wa
sera za kiuchumi na maendeleo, na inatumika katika kuangalia uboreshaji
wa hali ya maisha ya watu.


Alipongeza Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kufanya kazi
kwa weledi na ikiwemo kufanya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi
miaka mitatu kabla ya zoezi la kuhesabu watu kufanyika kama miongozo ya
kimataifa inavyoelekeza.


“Mataifa mengi ya Afrika yanakuja
kujifunza hapa Tanzania jinsi Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyotekeleza
majukumu yake kwa ufanisi hali iliyowezesha hata kuanza kwa zoezi hili
la utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili yan Sensa ya watu na
makazi ya mwaka 2022” Alisisitiza Mgoi


Akifafanua amesema kuwa viongozi
Viongozi katika ngazi zote hapa nchini wanapaswa kutoa ushirikiano kwa
watafiti kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakapokuwa wakitekeleza jukumu
la utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu ikiwa ni maandalizi ya sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2022 itakayofanyika hapa nchini.


Aliongeza kuwa Sensa hiyo
inatarajiwa kufanyika kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA na hivyo
kupunguza gharama kuanzia katika hatua za utengaji wa maeneo hadi
utekelezaji wa zoezi la sensa mwaka 2022.


Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa
Serikali Dkt Albina Chuwa aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa
kuendelea kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo
kuanza kwa zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa 
ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.


Aliongeza kuwa Ofisi yake inapata
ushirikiano wakutosha katika mamlaka za Serikali za Mitaa hali
inayowezesha kutekelezwa kwa ufanisi kwa zoezi hilo katika Wilaya ya
Bahi, Kondoa na Chamwino ambapo kwa Bahi tayari limekamilka pamoja na
Sehemu ya Wilaya ya Kondoa.


Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia
Bi Elizabeth Talbert amesema kuwa wataendelea kusaidia juhudi za
Serikali katika kufanikisha Sensa ya mwaka 2022 ili kuchochea maendeleo
kwa kuwa Benki hiyo hutumia takwimu hizo katika kusaidia miradi ya
maendeleo.


Zoezi la kutenga maeneo ya
kuhesabia watu  kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022
mkoani Dodoma limekamilika katika Wilaya za Bahi na Chamwino pamoja na
Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini na hivi sasa linaendelea katika
Halmashauri ya Kondoa mjini. 


Kwa kawaida, Sensa ya Watu na
Makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi. Sensa ya mwisho kufanyika
humu nchini ilikuwa mwaka 2012.