Serikali yaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kutoa ajira vijijini

 

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe za
uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa
Pili uliofanyika tarehe 01/08/2021 katika Kijiji cha Nalasi Wilaya ya
Tunduru Mkoa wa Ruvuma.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani akitoa maagizo kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi
kuhakikisha kuwa kifaa mbadala cha wiring UMETA kinapatikana ili
wananchi wasiomudu gharama za wiring waweze kuvitumia kwa ajili ya
kuunganishiwa umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia
Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge akiongea na umati wa wananchi wa Kijiji
cha Nalasi kilichopo Wilaya ya Tunduru ambako uzinduzi wa Mradi wa
Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliofanyika
tarehe 01/08/2021.

Watoto wakifuatilia matukio ya uzinduzi.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani akiwakabidhi wazee kifaa cha UMETA ambacho ni mbadala wa
wiring ili waweze kuunganishiwa umeme katika nyumba zao.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani akiwa na Mkuu wa Ruvuma Brigedia Jenerali,Balozi Wilbert
Ibuge pamoja na viongozi mbalimbali wakikata utepe kuashiria uzinduzi
wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili
ngazi ya mikoa katika Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika kijiji cha
Nalasi Wilaya ya Tunduru Agosti 1,2021.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani akiwa na Mkuu wa Ruvuma Brigedia Jenerali,Balozi Wilbert
Ibuge pamoja na viongozi mbalimbali wakipiga Makofi mara baada ya
kuzindua Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa
Pili ngazi ya mikoa katika Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika kijiji cha
Nalasi Wilaya ya Tunduru Agosti 1,2021.

………………………………….

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.
Medard Kalemani ameagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya
kusambaza umeme vijijini kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana waliopo
katika vijiji ambapo miradi hiyo inatekelezwa.

Dkt. Kalemani alitoa agizo  wakati
wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko
wa Pili ngazi ya mikoa katika Mkoa wa Ruvuma uliofanyika Agosti 1,2021
katika kijiji cha Nalasi Wilaya ya Tunduru.

“Wakandarasi chukueni vibarua
kutoka katika vijiji ambavyo mnapeleka umeme” alisema na kuongeza kuwa
lengo ni kufanya miradi hiyo iwe na tija kwa kuwashirikisha wananchi
katika kipindi cha utekelezaji wa mradi.

Aidha, Mhe. Kalemani amesema
Serikali itatumia zaidi ya Shilingi bilioni 71 kwa ajili ya kusambaza
miundombinu ya umeme katika vijiji 265 ambavyo havina huduma ya nishati
hiyo katika Mkoa wa Ruvuma.

“Katika Mkoa wa Rvuma, vijiji
vyenye umeme ni 289 kati ya 554. Kwa kutambua hilo leo ninawakabidhi
wakandarasi waushambulie Mkoa wa Ruuma na kuhakikisha vijiji vyote
vilivyosalia 265 vinapatiwa umeme kupitia mradi huu. Nipende kutoa rai
kwa Watanzania wote kuwa kila Mtanzania atapata Nishati ya Umeme”
alisema Waziri Kalemani.

Waziri Kalemani alisema kuwa
Wilaya ya Tunduru ambako Mradi umezinduliwa kuna vijiji 85 ambavyo hadi
sasa bado havijafikiwa na huduma ya umeme na kwa kutambua hilo, Serikali
imetenga  takribani Shilingi bilioni 23.52 kwa ajili ya kuvifikishia
umeme vijiji hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Brigedia Jenerali, Balozi Wilbert Ibuge aliwataka wananchi
wasihujumu miundombinu ya kusambaza umeme kwa kuiba nyaya na vifaa
vingine na wawe walinzi wa miundombinu hiyo.