Serikali yaanza kuwatambua wachunaji wa ngozi kisheria, yatoa onyo kwa wasiyokuwa na leseni

Na. Edward Kondela
Serikali imesema itasimamia sheria ya ngozi nchini ya mwaka 2008 ili
kuhakikisha zao hilo linaongezewa thamani kwa kuhakikisha inawatambua
rasmi wachunaji wa ngozi na kuzifungia machinjio na viwanda vya ngozi
visivyokuwa na wachunaji wa ngozi wanaotambulika kisheria.

Hayo yamebainishwa jana (23.01.2020) Mjini Morogoro na Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati wa hafla fupi ya kuzindua
rasmi mafunzo ya uchunaji ngozi nchini pamoja na kukabidhi leseni kwa
wahitimu 161 wa mafunzo ya uchunaji ngozi kutoka katika Manispaa ya
Morogoro ambao wametakiwa kufanya kadi kwa weledi mkubwa na kutaka
Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kuhakikisha inaendeleza
elimu hiyo katika ngazi ya wilaya.

“Ninaiagiza LITA kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ieneze katika
wilaya zote mafunzo haya ili wachunaji wa ngozi wapate vitambulisho ili
tusiweze kukwamisha shughuli za uchunaji wa ngozi katika wilaya zetu,
mkakati wa serikali na mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ni kuona
kwamba hatuendelei kutumia fedha zetu kuagiza bidhaa za ngozi kutoka
mataifa ya nje kuleta hapa Tanzania, lazima tujitosheleze sisi wenyewe
na tayari ngozi zetu ziwe zimetengenezwa katika hatua ya mwisho pamoja
na kutengeneza bidhaa za ngozi, tumeamua kusimama imara bidhaa za ngozi
zianze kutengenezwa katika utaratibu unaotakiwa.” Amesema Mhe. Ulega

Mhe. Ulega amesema Sheria Na. 18 ya Mwaka 2008 Kifungu Na. 15 katika
sheria inayosimamia biashara ya ngozi, inawataja wataalam wa uchunaji wa
ngozi na kwamba kama machinjio haina wataalamu wa uchunaji ngozi au
kiwanda hakina wataalam sheria inakataza.

Amefafanua kuwa sheria hiyo inaeleza wazi kuwa ikiwa mtu anafanya kazi
ya kuchuna ngozi bila kutambuliwa rasmi kisheria zipo adhabu ikiwemo ya
kupelekwa mahakamani ambapo kifungu kidogo cha pili kinabainisha kuwa
atakayebainika kufanya kazi ya kuchuna ngozi bila kutambuliwa kisheria,
atalipishwa faini ya shilingi Milioni Moja au kifungo kisichozidi Miezi
Sita au adhabu zote mbili.

Naibu waziri huyo amefafanua kuwa maandalizi ya Tanzania ya viwanda
ambayo ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano ya kukuza viwanda
nchini ambavyo vinategemea malighafi zinatokana na kilimo, mifugo na
uvuvi, ngozi ni malighafi muhimu katika kutengeneza bidhaa zitokanazo na
zao hilo.

“Zao la ngozi limekuwa zao muhimu katika sekta ya mifugo kwa kuliingiza
pato taifa kwa mwaka 2019/20 kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi
Desemba, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ngozi
imepata jumla ya makusanyo ya Shilingi Bilioni 5.3, aidha zao la ngozi
limeendelea kutoa ajira na kukuza kipato kwa watanzania na
wafanyabiashara wa ngozi.” Amefafanua Mhe. Ulega

Awali akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao
ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Bw. Gabriel Bura amesema mafunzo yaliyotolewa ya uchunaji ngozi kwa
washiriki 176 ni utekeleaji wa sheria baada ya kukutana na wadau
mbalimbali ambao wamebainisha kuwa ngozi ya Tanzania ina ubora hafifu 
kutokana na sababu mbalimbali.

“Ngozi inaharibika kwa mfugaji kwa asilimia 30 kutokana na kupiga mfugo
chapa katika maeneo yasiyofaa, mnyama kupita kwenye vichaka, lishe duni
na magonjwa ya kupe na ndorobo, aidha asilimia 50 ngozi inaharibika
kwenye machinjio namna mnyama anavyochinjwa na namna mchunaji
anavyoichuna ngozi hiyo pamoja na vifaa anavyotumia.” Amesema Bw. Bura

Bw. Bura amesema mafunzo ya uchunaji ngozi na utoaji wa leseni tayari
yametolewa katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na katika
Manispaa ya Morogoro na yanatarajia kuendelea Mwezi Februari mwaka huu
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ili wachunaji wa ngozi waweze
kufanya kazi kwa mujibu kwa sheria.

Bw. Mapinduzi Ernest akizungumza kwa niaba ya wachunaji wenzake wa ngozi
katika Manispaa ya Morogoro waliopatiwa mafunzo na hatimaye kukabidhiwa
leseni ameishukuru serikali kwa kutoa elimu ya uchunaji bora wa ngozi
ili kupandisha thamani ya ngozi ambayo inahitajika katika viwanda
mbalimbali hapa nchini kutengenezea bidhaa.

Amesema ngozi ya mnyama ikichunwa vizuri itatoa tathmini ya ubora wa
ngozi na kuiomba serikali kuhakikisha elimu hiyo inakuwa endelevu ili
malighafi ya ngozi iweze kuwa bora zaidi.