Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akishuhudia namna wataalam wa
Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI), wakiwa kwenye moja ya hatua za
kuzalisha chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo ambapo Waziri Ndaki
ameridhishwa na utendaji kazi wa taasisi hiyo na kusisitiza kuwa chanjo
zinazozalishwa katika kituo hicho zinatosheleza mahitaji ya nchi na
kuwataka wafugaji kuchanja mifugo yao. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akishuhudia
chanjo mbalimbali zinazozalishwa na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI)
iliyo chini ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), wakati
alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi hiyo iliyopo
Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ili kushuhudia chanjo zinazozalishwa hapa
nchini. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza) akikagua mitambo
mbalimbali iliyofungwa katika kiwanda cha kuzalisha chanjo HESTER
ambacho kinajengwa Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani, ambapo Waziri Ndaki
amesema uwepo wa viwanda vingi vya chanjo hapa nchini kutasaidia nchi
kuwa tayari kukabiliana na magonjwa yoyote ya mifugo pindi mlipuko wa
magonjwa ukitokea. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kulia) akishuhudia
namna kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama TAN CHOICE kinavyofanya
kazi wakati alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda hicho kilichopo
Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na kuwataka wafugaji waanze kubadilisha
fikra zao na kufuga kisasa kwa kuwa viwanda vya namna hiyo vinahitaji
nyama bora ili kukidhi soko la kimataifa. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akiangalia
namna nyama ya mbuzi ilivyohifadhiwa katika chumba chenye baridi kali
kabla ya taratibu nyingine za kusafirisha nyama hiyo kwenda nje ya nchi.
Waziri Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kiwanda cha
kuchinja na kuchakata nyama TAN CHOICE kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani
Pwani. (Picha na Edward Kondela – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema Tanzania ina chanjo za
kutosha dhidi ya magonjwa ya mifugo na kuagiza wafugaji wote nchini
pamoja na maeneo ambayo serikali inafuga kuhakikisha mifugo yao
inachanjwa ili kuondokana na magonjwa hayo.
Akizungumza
jana (24.12.2020) mara baada ya kutembelea Taasisi ya Chanjo Tanzania
(TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya
siku mbili mkoani humo, Waziri Ndaki amesema ili kuhakikisha Tanzania
inakuwa na mifugo bora inayokidhi soko la kimataifa ni lazima mifugo
ichanjwe dhidi ya magonjwa ili yapatikane mazao bora ya mifugo.
“Tunayo
chanjo ya kutosha hivyo niwatake wafugaji wote ikiwa ni pamoja na sisi
serikali kwenye maeneo ambayo tunafuga tuchanje mifugo yetu ili tupate
mifugo iliyo bora, tunataka sasa nchi yetu iende kwenye ubora badala ya
uwingi wa mifugo, ili tupate nyama bora na maziwa bora kwa maana ya
mazao bora ya mifugo ili tuweze kuuza katika soko la kimataifa.” Amesema Mhe. Ndaki
Katika
ziara hiyo kwenye taasisi ya TVI, Waziri Ndaki alitaka kufahamu namna
agizo alilolitoa hivi karibuni la ng’ombe waliopo kwenye ranchi 14 za
taifa kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu kutokana na baadhi ya
mifugo hiyo kuathiriwa na ugonjwa huo katika Ranchi ya Kongwa iliyopo
Mkoani Dodoma, ambapo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya
Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo inaisimamia TVI, Dkt. Stella Bitanyi
amesema chanjo zimesambazwa kutokana na mahitaji ya ranchi hizo na sasa
wapo katika hatua ya chanjo hizo kuwafikia majirani wa ranchi hizo ili
kuweza kuchanja ng’ombe wao.
Aidha,
Waziri Ndaki amejionea ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha
HESTER kilichopo Wilayani Kibaha na kupongeza hatua mbalimbali ambazo
zimefikiwa katika ujenzi huo na kusema mara kiwanda hicho kitakapoanza
kufanya kazi Mwezi Aprili Mwaka 2021, kitasaidia kuongeza wigo wa uwepo
wa chanjo nyingi hapa nchini na kusaidia endapo magonjwa ya mifugo
yatajitokeza.
“Hii
inaonesha umuhimu wa kuwa na chanjo tayari kwa ajili ya mifugo yetu
yote ili ikitokea magonjwa ya milipuko tuweze kupata mahali pa kusaidiwa
kwa karibu na pengine kwa bei nafuu kwa kuwa chanjo hizi zitakuwa
zinazalishwa hapa nchini.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika pia katika kiwanda cha
kuchinja na kuchakata nyama cha TAN CHOICE kilichopo Wilayani Kibaha, na
kubainisha kuwa umuhimu wa uwepo wa viwanda hivyo kutasaidia
kubadilisha fikra za wafugaji kwa kuingia kwenye ufugaji bora.
Kuhusu
changamoto ya vibali vya kuingiza nyama zilizochakatwa kwenye baadhi ya
nchi kutoka Tanzania, Waziri Ndaki amesema wizara itawasiliana na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Wizara ya
Viwanda na Biashara ili kufahamu changamoto zinazovikabili baadhi ya
viwanda kushindwa kusafirisha nyama kwenda baadhi ya nchi kutokana na
kukosa vibali vya kuingiza nyama hizo kutoka Tanzania.
Pia,
amefafanua kuwa uwepo wa viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama nchini
kunazidi kusaidia kukuza biashara ya mifugo nchini na kuongeza wigo wa
soko la mifugo hivyo ni muhimu kwa wafugaji kuanza kuhakikisha wanakuwa
na mifugo iliyo bora ili waweze kuuza mifugo yao kwa bei nzuri na waweze
kunufaika kiuchumi na taifa pia liweze kupata mapato ya kutosha kupitia
biashara ya mifugo.
Awali
akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki amekutana na mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist
Ndikilo ambapo wamezungumza mambo mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo
na uvuvi.
Katika
mazungumzo hayo Mhandisi Ndikilo amesema kwa sasa migogoro ya wakulima
na wafugaji imepungua kwa kiasi kikubwa huku akitaka juhudi zaidi
zifanyike katika kuwapatia wafugaji elimu ya kuwa na mifugo michache na
yenye tija badala ya kuwa na mifugo mingi ambayo haitoshi kutokana na
uwepo wa maeneo ya kufugia.
Kwa
upande wake Waziri Ndaki amesema changamoto zinazohusu wizara
atahakikisha zinafanyiwa kazi ili sekta za mifugo na uvuvi ziwe endelevu
na kuondokana na migogoro isiyo na tija kwa taifa.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya
siku mbili Mkoani Pwani, ambapo katika siku ya kwanza (23.12.2020)
alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji Wilayani Rufiji na
kuwataka kuheshimu maeneo waliyopewa na uongozi wa mkoa kwa ajili ya
ufugaji na kuacha kuingia katika maeneo ya wakulima.