Serikali yasitisha zoezi la uokoaji waliofukiwa na kifusi mgodi imalanguza mkoani geita

1.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika maeneo hayo
wakiwa kwenye eneo la tukio siku ya tarehe 1/10/2019 walipofukiwa

Na Issa Mtuwa “WM” – Geita

Majonzi na huzuni vimetawala kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo wa
Imalanguza wilaya ya Geita kata ya Lwamgasa katika Kijiji cha
Imalanguzu, mara baada ya kuwasili Naibu Waziri wa Madini Stanslausi
Nyongo mgodini hapo akiwa na viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya
Madini, uongozi wa mkoa na viongozi wa dini kwa ajili ya kwenda
kusitisha shughuli za uokoaji wa wachimbaji wadogo wawili Karos Msukuma
Paulo mwenyeji wa Chato na Kulwa Joseph Mahungija mwenyeji wa Busolwa
Nyang’wale waliofukiwa kifusi siku ya tarehe 1/10/2019.

Usitishaji wa zoezi hilo umefanyika tarehe 9/11/2019 ikiwa ni siku 39
tangu wachimbaji hao wafukiwe na kifusi kutokana na uwepo wa changamoto
mbalimbali zilizo jitokeza katika kipindi chote cha uokoaji. Ripoti
maalam ya timu ya wataalam wa uokoji imeeleza kuwa kumekuwa na
changamoto nyingi wakati wote wa ukoji zilizopelekea kuwa na ugumu wa
kuwaokoa wachimbaji hao.

Akiwasilisha taarifa ya wataalam wa uokoaji iliyoishauri serikali
kusitisha kwa zoezi hilo la uokoaji kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus
Nyongo,  mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga amemwambia Naibu
Waziri wa Madini kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza wakati wa
uokoaji ni pamoja na uwepo wa maji chini ya mgodi, mwingiano wa magogo
mbalimbali chini ya shimo la mgodi, na kutokuwa na usalama katika eneo
hilo hata kwa vyombo vya uokoaji.

Maganga aliongeza kuwa, kulikuwa na wataalam wa makundi mbalimbali ya
uokoaji na vifaa vya kutosha kutoka kwa jeshi na uokoaji, mgodi wa
dhahabu wa Geita (GGM), na makampuni mengine kutoka kwenye migodi
mbalimbali, lakini pamoja na juhudi zote hizo imeshindikana kupatikana
kwao.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa  siku ya tukio hilo, kwenye shimo
hilo kulikuwa na wachimbaji 5 ambapo 3 kati yao waliokolewa siku hiyo
hiyo na wawili hawakuweza kupatikana hadi zoezi hilo la uokoaji
linasitishwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri Nyongo, akiongea kwa masikitiko na
majozi kwenye hadhara hiyo, Nyongo amesema kwanza lililotokea ni bahati
mbaya na kwamba serikali imesikitishwa na tukio hilo na kwamba iko
pamoja wafiwa na wachimbaji wote.

Ameongeza kuwa, serikali inathamini sana hata uhai wa mtu mmoja
kuliko dhahabu au madini yote yaliko chini na ndio maana inasisitiza
wachimbaji kuchimba kwa kufuata utaratibu na sharia ili wachimbe kwa
kuzingaatia usalama ili kuepukana na majanga kama hayo.

Nyongo ametowa kauli ya serikali ya kuhitimisha shughuli za uokoaji
na kutoa maelekezo kuhusu eneo hilo ambalo wachimbaji hao wamefukiwa na
kifusi.

“Na sasa tunakwenda kufanya ibada ya kwenda kuwazika wenzetu, viongi
wetu wa dini wako hapa watatuongoza katika ibada hiyo kwa ajili ya
maombi. Natamka kuwa, shughuli zote za uchimbaji katika eneo ambalo
tunaamini kuwa ndipo wezentu hawa wapo, basi eneo hilo litambuliwe rasmi
kuwa ndio kabuli lao na kama kuna undelezaji wa shughuli ya uchimbaji
utaendelea katika eneo lingine na kwa utaratibu mwingine.” alisema
Nyongo.

Nyongo pia alitoa maagizo kwa afisa madini mkazi mkoa wa Geita na
timu yake kusimamia usitishwaji wa shughuli za uchimbaji katika eneo
hilo mpaka pale hatua za uzingatiaji usalama ziwe zimefuatwa ili
kuepusha ajali nyingine.

Kwa upannde wake Mchungaji Nuhu Suleman alie ongoza ibada hiyo ya
kuwaombea marehemu alisema, hapana budi kumshukuru mungu kwa kila jambo
na kila jambo hukusudiwa na mungu.
 Amewakumbusha waumini wote kumuelekea
mungu kwani yeye ndie mwenye upekee na ufalme na kwamba maisha ya
binaadamu yana ukomo ni vyema kila mmoja akajiandaa na safari hiyo.