Shehena ya mifuko isiyokidhi viwango yakamatwa

Ofisi
ya Makamu wa Rais inaendelea kusimamia marufuku ya katazo la matumizi
ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha Kitaifa. 


Kwa
siku za hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la uzalishaji, utengezaji na
uingizaji na usambazaji wa mifuko isiyokidhi viwango vilivyowekwa na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kikosi
kazi cha Kitaifa cha kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na
Kamati za Mikoa na Wilaya wanaendesha oparesheni maalumu nchi nzima kwa
lengo la kusaka mifuko isiyokidhi viwango.

Tarehe
30/10/2019 NEMC ilikamata marobota 21 katika Wilaya ya Misenyi, Mkoani
Kagera na marobota 7 Mkoani Arusha ambayo yanashikiliwa katika kituo cha
polisi cha Arusha. Upelelezi wa mashauri haya bado unaendelea.

Tarehe
4/11/2019 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi kwa Mazingira (NEMC)
kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza
wamekamata shehena ya mifuko isiyokidhi viwango gunia 8 yenye thamani ya
Shilingi 10,000,000/-  Mifuko hiyo iliingia kupitia bandari bubu ya
Bwiru jijini Mwanza ikitokea nchi jirani. Watuhumiwa watafikishwa
mahakamani na mifuko hiyo itateketezwa kwa mujibu wa sheria kama
itakavyoelekezwa na NEMC.

Ofisi
ya Makamu wa Rais, inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha
na uingizaji, usambazaji na uuzaji wa mifuko mbadala kuhakikisha
wanazingatia matakwa ya Sheria. Aidha, wafanyabiashara wanasisitizwa
kuacha kuzalisha, kuingiza nchini, kuuza na kusambaza mifuko isiyokidhi
viwango. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote wanaokiuka
agizo hilo.