Tanesco saccos kujenga jengo la ofisi

     

Chama
cha Ushirika wa Akiba na Mikopo TANESCO kimeanza mchakato wa shughuli
za ujenzi wa jengo la ofisi baada ya kukamilika kwa taratibu za
kuhamisha hati ya kiwanja kutoka Chama cha Ushirika wa Nyumba Mwenge
(MHCS) kuja TANESCO SACCOS.


Akisoma
Taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu uliofanyika kwa siku mbili tarehe 14 –
15 Novemba, 2020 Jijini Dar Es Salaam, Mwenyekiti wa TANESCO SACCOS,
Somoe Nguhwe amesema chama kimempata Mshauri Mwwelekezi wa mradi wa
ujenzi (Consultant) ambaye ameanza kazi kwa kuandaa michoro na kuandaa
nyaraka za kumpata mjenzi (Contractor).


Mrajis
wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya
Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, amewapongeza viongozi wa TANESCO SACCOS
kwa hatua ya kuanza taratibu za ujenzi wa jengo la ofisi.


“Nichukue
nafasi hii kuwasihi viongozi kuendelea na mchakato wa utekelezaji wa
mradi huo wa ujenzi la jengo la ofisi, ili kukuza taswira ya Chama na
kuokoa gharama zinazoingiwa na Chama kulipa kodi ya pango,” amesema Dkt.
Ndiege


Hata
hivyo, Dkt. Ndiege amesema kuwa ujenzi huo lazima uzingatie maslahi ya
wanachama na kutowafanya wanachama kukosa mikopo kwa kisingizio cha
kujenga. Pia ujenzi huo ufuate kikamilifu sheria na miongozo ya manunuzi
na uwekezaji kwenye vyama vya ushirika.


Mrajis
amekipongeza Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo TANESCO kwa kuwa
kati ya vyama vichache vilivyoweza kupata Hati Safi na kudhihirisha kuwa
chama hicho kimeendelea kusimamia mali za wanachama kwa uaminifu.


Dkt.
Ndiege amewapongeza viongozi na wanachama wa TANESCO SACCOS kwa hatua
madhubuti wanayoichukua ya uwekezaji katika taasisi za ndani ya Sekta
kwa maana uwekezaji katika ya Benki wa Ushirika (KCBL).



“Niwahakikishie kwamba serikali kupitia Benki Kuu (BoT) na Tume ya
Maendeleo ya Ushirika (TCDC) imejipanga kusimamia benki hii muhimu kwa
wanaushirika na watanzania kwa ujumla. Niwahakikishie hii ni fursa
muhimu sana ya uwekezaji,” amesema Dkt. Ndiege.


Mkutano
Mkuu wa TANESCO SACCOS kwa mwaka huu ni wa uchaguzi ambapo Wajumbe
watachagua viongozi ambao watasimamia Chama kwa kipindi cha miaka
mitatu. Dkt. Ndiege amewaasa wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa makini sana
kuhakikisha kuwa wanachagua viongozi mahiri ambao wataendeleza kazi
nzuri iliyofanywa na Uongozi unaomaliza muda wao.


“Uongozi
wa Chama ndiyo Dira kwa maendeleo ya Chama kwani kama uongozi ukiwa
legelege uwezekano wa kuua Chama ni mkubwa kwani wanachama watakosa
imani. Hivyo kabla ya kuchagua hakikisha unatafakari usichague kwa
ushabiki,” amesema Mrajis.


Kwa
kuzingatia utendaji mzuri wa bodi iliyo maliza kazi yake, na Kwa mujibu
wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013, Kifungu cha 137
kinampa Mrajis mamlaka ya kuteua mjumbe / wajumbe wa Bodi ambao ataona
wanafaa kushika nafasi ya ujumbe huo kwa maslahi ya umma na chama kwa
ujumla.


Kwa
kuzingatia mamlaka haya aliyonayo Mrajis, amemteua Bi. Somoe Nguhwe
ambaye atakuwa sehemu ya Bodi ya TANESCO SACCOS kwa lengo la kuimarisha
utendaji kazi, ubora wa huduma pamoja na kuendelea kuimarisha Sekta ya
Ushirika wa Akiba na Mikopo nchini na nje ya nchi. Aidha, Lengo kubwa ni
kuendeleza ushirikiano kwenye taasisi zetu za Ushirika nchini (SCCULT)
pamoja na ushirikiano wa nje ya nchi (ACCOSCA na WOCCU).


Bi.
Somoe Nguhwe amekuwa mwanachama mwenye uzoefu mkubwa na amesomea na
kufanya kazi za masuala ya ushirika kwa kipindi kirefu tangu Mwaka 1984.
Mwanachama huyu amekuwa na uzoefu kwenye nafasi ya uongozi na utendaji
kazi kwenye SACCOS tangu Mwaka 1981.


Dkt.
Ndiege amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Tanzania imedhamiria kuimarisha utendaji kazi wa Vyama vya Ushirika
nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka taswira nzuri ya Ushirika kwa
umma ili wananchi wengi waweze kuvutiwa na kuendelea kutumia huduma na
bidhaa zinazotolewa na Vyama vya Ushirika nchini.