TANESCO yajipanga kufikia lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa ifikapo 2030.

Na, Egidia Vedasto

APC Media, Arusha.

Shirika la umeme Nchini (TANESCO) limejipanga kuhakikisha linafikia lengo la kuwapatia wananchi wake umeme wa uhakika ili kuendana na Dira ya maendeleo ya upatikanaji wa nishati ya uhakiaka kwa watu wapatao milioni 300 kati ya 600 kwa nchi za Afrika.

Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Nishati uliokutanisha wadau mbalimbali, Naibu Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Mhandisi Costa Rubagumya amesema ili kufikia mkakati huo uliowekwa, Shirika limejipanga kuhudumia wateja milioni moja na laki sita (1,600,000)kwa mwaka badala ya wateja laki tano (500,000)kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.

Aidha Mhandisi Rubagumya ameongeza kwamba mkutano huo unajadili mbinu na njia zitakazosaidia kufikia malengo ya Dira ya mwaka 2030, ambapo kwa Tanzania inatarajiwa kuwapatia wananchi milioni 8.3 kufikia mwaka 2030.

“Tunachokijadili hapa ni namna tutakavyoshirikiana katika uzalishaji wa umeme, usafirishaji na usambazaji na hata kufikia wale ambao walikuwa hawapati huduma zetu” amefafanua Mhandisi Rubagumya.

Wadau wa Nishati ya Umeme katika Mkutano uliofanyika Jijini Arusha

Kwa upande wake Frank Mmbando aliyeiwakilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, amesema kwamba Serikali ya Mkoa wa Arusha imekuwa ikiweka mazingira wezeshi ya nishati ili kuhakikisha shughuli za uwekezaji zinafanikiwa.

Pia amefafanua namna Bwawa la Nyerere linvyoendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa Megawat 2115 na kuingia kwenye Grid.

“Nchi yetu imekuwa kinara na inaendelea kutajwa kwa wingi, hii ni baada ya kuanza biashara ya kuuza umeme katika nchi mbalimbali kama Kenya, Ethiopia, Uganda na Burundi” amefafanua Mmbando.

Vilevile Mkurugenzi mtendaji wa shirika la umeme la nchini Kenya Joseph Siror amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeandaa mpango kwamba nishati zote zinazozalishwa, ziwekwe katika soko, ili wananchi waweze kununua na kutumia kwa bei nafuu.

“Bwawa la Nyerere Nchini Tanzania litakuwa mkombozi kwa kutoa umeme wa kutosha, na kusaidia Jumuiya hii hususan nchi zile ambazo hazijapata uwezo kama huu” ameeleza Siror.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) anayehusika na masuala ya uzalishaji wa umeme Mhandisi Costa Rubagumya
Mkurugenzi Mtendaji shirika la umeme nchini Kenya Joseph Siror