Tanzania inatarajia kupata dola za marekani milioni 500 kwa ajili ya mradi wa elimu

Kutoka kulia ni Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. (Mb)  Philip Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango
Zanzibar Mhe. Mohamed R. Abdiwawa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango Zanzibar Bw. Khamis M. Omary wakiwa kwenye mazungumzo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (hayupo pichani) kuhusu miradi ya
maendeleo nchini Tanzania

.
Kutoka kulia ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kundi la  Afrika Bi Anne
Namara Kabagambe na Mshauri Mwandamizi kundi la Afrika Bw. Zarau
Kibwe akielezea mafanikio aliyoyaona alipotembelea miradi ya Maendeleo
Tanzania.  (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)


Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, Washington Dc

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) amefanya mazungumzo na  Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Dunia anayewakilisha nchi za Afrika Bi. Anne Namara
Kabagambe, Mjini Washington DC, Marekani.

Mazungumzo hayo yalilenga katika
kubadilishana uzoefu juu ya utekelezaji wa Sera mbalimbali za fedha na
namna uchumi wa Dunia unavyoendeshwa.

Katika mazungumzo hayo baadhi ya
miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa(SGR), ujenzi wa Bwawa kubwa la
kuzalisha umeme la mto Rufiji, mradi wa elimu,na miradi ya Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF), ilijadiliwa.  

Dr. Mpango alieleza dhamira ya
Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ya kuinua kiwango cha elimu, kwa kutafuta fedha zaidi na mikopo ya
masharti nafuu ambayo itaelekezwa kwenye elimu.

‘’Katika Mradi wa Elimu
unaotarajiwa kuwasilishwa Benki ya Dunia mwezi Novemba, 2019,
tunatarajia kupata dola za Marekani milioni 500, na nimemuomba Bi. Anne
Namara Kabagambe azidi kusisitiza ili Taifa liweze kupatafedha hizi kwa
wakati, na tunaamini kwamba fedha hizo zitaidhinishwa na Benki ya Dunia
kama tunavyotarajia.”
Alisisitiza Dkt Mpango.

Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango
alisema pamoja na miradi ya Elimu, Sekta  ya nishati ya umeme pia ni
muhimu katika kuinua uchumi wa nchi kwa sababu ukipatikana umeme wa
kutosha utasaidia kwa vitendo agenda ya uchumi wa viwanda kwa kuongeza
thamani ya mazao na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini.

Aliiomba Benki ya Dunia na Shirika
la Fedha la Kimataifa zisaidie kwenye miradi ya mikubwa inayotekelezwa
na Serikali hasa katika sekta ya umeme na miundombinu.

Aidha Dkt. Mpango alieleza kuwa
hivi karibunii Benki ya Dunia iliipatia Tanzania mkopo wenye masharti
nafuu wa dola za Marekani milioni 450 kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu
ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii- TASAF, awamu ya tatu.

“Hivyo kupitia miradi miwili ya Elimu na TASAF, Tanzania inatarajia kupata dola za Marekani milioni 950”. Aliongeza Dkt. Mpango

Kwa upande wa Benki ya Dunia Bi.
Anne Namara Kabagambe alielezea kufurahishwa na utekelezaji wa miradi
inayofanyika Tanzania kwani alipata fursa ya kuona miradi mbalimbali
ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na miradi inayotekelezwa
na TASAF, na kuelezea kuwa ni miradi ya mfano na kwa nafasi yake
ataendelea kuitangaza miradi hiyo ili Tanzania iweze kupata fedha zaidi
ya kutekeleza miradi hiyo.

Dkt. Mpango anaongoza ujumbe wa
Tanzania kwenye Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha
Dunia IMF ambapo amesema mikutano hiyo ni muhimu kwa kuwa nchi itapata
fursa ya kuweza kujadiliana na Taasisi hizi za IMF na WB kuhusu  miradi
wanayofadhili.

Aidha, kupitia mikutano hiyo
vipaumbele vya nchi vitaelezwa na kupitia changamoto zilizopo kwa sasa,
kutetea maslahi mapana ya Tanzania katika utekelezaji wa programu za
maendeleo na mabadiliko ya kimfumo katika uendeshaji wa uchumi
kutegemeana na mwenendo wa Dunia unavyokwenda.

 Alisisitiza kuwa nchi inapata
uzoefu wa nchi nyingine wanavyotekeleza na kusimamia program zao na wao
pia kuweza kuzieleza nchi nyingine namna ambavyo Tanzania inatekeleza
programu mbalimbali za kimaendeleo.