Rc mnyeti aunguruma kiteto

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Kijungu Wilayani Kiteto.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa Kata ya Lengatei Wilayani Kiteto.
Wananchi wa Kata ya
Dongo Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander
Pastory Mnyeti alipotembea eneo hilo.
…………………
MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Pastory Mnyeti ameunguruma Wilayani Kiteto kwa
kuagiza wakulima waheshimu eneo la malisho la wafugaji wa Amei na
wakulima wa Kata ya Dongo walionyang’anywa maeneo yao warudishiwe kwani
hawakupewa eneo mbadala. 
Mnyeti alitoa maagizo hayo Wilayani Kiteto alipotembelea maeneo hayo kwenye ziara yake ya siku tano ya wilaya ya Kiteto. 

Alisema wakulima wa Amei wasiingilie eneo la mifugo kwani limewekwa kwa ajili ya wafugaji. 

“Mlishajipangia
wenyewe kuwa lile ni eneo la mifugo hivyo wakulima muache kusogelea hapo
mtasababisha vurugu ili hali mlijiamulia wenyewe matumizi ya ardhi
yenu,” alisema Mnyeti. 
Alisema kwenye eneo
la Dongo kuna baadhi ya wakulima walifukuzwa kwenye sehemu yao bila
kupewa eneo mbadala hivyo warudi katika eneo lao. 

“Wakulima walifukuzwa
bila kupewa eneo lingine hivyo rudini ili muendeshe maisha yenu kama
ilivyokuwa awali kwani hamkupewa maeneo mbadala ya kulima,” alisema
Mnyeti. 
Pia, aliwataka
wafugaji na wakulima kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi
waliyojiwekea ili kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji. 

“Heshimuni mpango huo
mlioamua wenyewe kwani mfugaji akiheshimu sehemu ya wakulima na
wakulima wakiheshimu eneo la wafugaji hakutatokea tatizo lolote,”
alisema Mnyeti. 
Mkuu huyo wa mkoa
alileta faraja kwa mkazi wa kijiji cha Zambia kikongwe aliyenyang’anywa
eneo na baadhi ya viongozi wa kijiji hicho. 

“Kuanzia sasa hivi
wewe mama rudi kwenye eneo lake la awali na mtu yeyote asikusumbue
mtendaji wa kijiji, kata na ofisa Tarafa mlindeni huyu mama asiguswe na
mtu,” alisema Mnyeti. 

Akiwa kwenye kata ya
Lengatei aliagiza mkazi wa eneo hilo Hassan Ramadhan kurudishiwa eneo
lake lililotaka kujengwa shule shikizi ili hali alishinda shauri lake
kwenye baraza la ardhi na nyumba la wilaya ya Kiteto. 

Lengo la ziara hiyo
ni kuzungumza na wananchi, kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero
na changamoto na kuyapatia majawabu na kuhamasisha wananchi
kujiandikisha ili waweze kupiga kura ya kuwachagua viongozi wa serikali
za mitaa.