Tanzania na angola kushirikiana katika eneo la mafuta, gesi na mapambano dhidi ya rushwa

Na Mwandishi Maalum Dodoma 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardusi Kilangi, jana 
 (Alhamisi) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa
Serikali ya Angola hapa Nchini, Mhe. Balozi Sandro Renato Agostinho de OLIVEIRA.
Mazungumzo baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Kilangi na Balozi Sandro Renato Agostinho de OLIVEIRA ambayo yamefanyika katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jijini Dodoma, yalijikita katika kuangaliana namna gani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania itakavyoshirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Angola.
Balozi wa Angola Mhe. Sandro Renato Agostinho de OLIVEIRA,
alimweleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi kwamba, Serikali yake, yaani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ingependa kushirikiana karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania katika maeneo kadhaa likiwamo namna ya kukabiliana na tatizo la rushwa.
"Tungependa (Angola) kuanzisha mahusiano na masharikiano baina ya Ofisi yako na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Angola.


Tunaamini kuna maeneo mengi ambayo tunaweza kubadilishana uzoefu likiwamo hili la kukabiliana na changamoto za rushwa". Akasema Balozi de OLIVEIRA.
Aidha Balozi huyo wa Angola alisema amefurahi sana kufika Jijini Dodoma kwa kuwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza.
 Kwa upande wake Profesa Adelarus Kilangi pamoja na kushukuru
kwa Balozi huyo wa Angola kumtembelea, alimweleza kwamba Ofisi yake ipo tayari kuanzisha mahusiano na mashirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Angola.
AG Kilangi pamoja na kukubaliana kushirikiana na kubadilisha uzoefu katika eneo la kukabiliana na rushwa, yeye alitaka ushirikiano pia katika eneo la mafuta na gesi na pia katika maeneo ya kujengeana uwezo na maarifa katika maeneo mbalimbali.
Itakumbukwa kwamba, Nchi ya Angola ni kati ya nchi chache za Bara la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinautajiri mkubwa wa mafuta na gasi na wanauzoefu wa kutosha eneo hilo.