TPHPA KUFIKIA MALENGO YA KUBORESHA AFYA ZA WALAJI.

Egidia Vedasto 

Arusha

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Nchini  TPHPA imeweka mikakati ya msingi inayolenga kuzalishwa mazao yasiyo na sumu ili kupanua wigo katika soko la dunia kwa mustakabali wa kulinda afya za walaji.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Wadau wa  TPHPA Jijini Arusha, Mkuu wa  Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyetarajiwa kuwa Mgeni Rasmi, ameipongeza mamlaka hiyo kwa jitihada zake kubwa za kuleta mabadiliko na uzalishaji wenye tija  katika sekta ya kilimo.

Aidha ameongeza kuwa, Sekta ya Kilimo ni mkombozi kwani inategemewa kuongeza ajira kwa jamii hususani vijana na wanawake, kuimarisha mfumo wa chakula na kuongeza pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii muhimu imeongeza bajeti kutoka Bilioni 970 kwa mwaka wa fedha  2023/2024 kufikia Tirioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hii yote ni kuhakikisha tunajiimarisha katika soko la dunia na kuzidi kuwa bora katika uzalishaji wa chakula cha kutosha”

“Nawasisitiza Mamlaka ya TPHPA kuhifadhi mbegu za asili, hii itasaidia kuepuka upotevu wa mbegu bora zinazotegemewa katika ushindani wa soko la dunia” amesisitiza Kaganda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPHPA Prof. Andrew Temu amesema kuna muelekeo wa mamlaka hiyo kutimiza malengo yake ya kuboresha afya za watu kutokana na juhudi na mikakati mbambali inayowekwa.

Ameongeza kuwa, TPHPA inatambua juhudi za serikali katika utekelezaji wa majukumu yao, ushauri na maelekezo muhimu yenye lengo la kuhakikisha mamlaka hiyo inaimarika na kuendelea kufanya vizuri.

“Tunaendelea na jitihada za kutanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji lakini pia kupambana na changamoto mbalimbali zikiwemo usugu wa viuatilifu, kupotea kwa vinasaba katika mimea ya asili, ubunifu na mbinu   juu ya viuatilifu sambamba na hayo tunajipanga kwa matumizi ya akili mnemba ili kuendana na Maendeleo ya Teknolojia lakini pia kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi” ameeleza Prof. Temu.

Mkurugenzi wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru ameeleza kuwa, mkutano huu umetoa fursa kwa wadau wa sekta ya kilimo kubadilishana uzoefu, changamoto na ushauri katika kuleta mageuzi kwa sekta hiyo.

“Naishukuru kamati ya kudumu ya Bunge, inayosimamia Wizara ya Kilimo, Viwanda na Biashara kwa kupitisha bajeti ambayo imetupa tumaini la kufikia malengo tuliyojiwekea TPHPA” ameeleza Prof. Ndunguru.

Mmoja wa wadau aliyeshiriki katika mkutano huo, Afisa kilimo Mohamed Hussein kutoka kampuni ya Agrimatco Tanzania LTD amesema wanashirikiana vyema na mamlaka ya TPHPA na wamekuwa wakipata elimu na  miongozo inayowasaidia kuboresha utendaji na utoaji huduma bora kwa wakulima.

“Hii mamlaka ni mkombozi wetu lakini pia inatuelekeza namna ya matumizi bora ya viuatilifu na jinsi ya kuwashauri wateja wetu ambao ni wakulima” amesema Hussein.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emanuel Kaganda akipata maelezo kutoka kwa kampuni ya Agromatico Tanzania Limited waliokuwa wakionyesha bidhaa wanazozalisha kwaajili ya wakulima katika maonyesho yaliyokuwa yakifanyika katika mkutano huo