Uamuzi wa mahakama kuhusu sheria ya mtoto kuolewa chini ya miaka 18

Mahakama
ya Rufani Tanzania imeitaka Serikali ya Tanzania kubadilisha vifungu
vya Sheria ya Ndoa inayoruhusu Mtoto wa Kike kuolewa chini ya miaka 18
ili kuweka usawa baina ya Mtoto wa Kike na Kiume.


Uamuzi
huo umesomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Eddie Fussi
ambapo alisema Mahakama ya Rufani inakubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu
iliyotolewa Julai 8, 2016.

Msajili
Fussi akisoma uamuzi huo ulioandikwa na Jopo la Majaji watatu ambao ni
Augustine Mwarija , Winfrida Korosso na Dk Mary Lavira amesema sheria
hiyo inakiuka Katiba na haiweki usawa baina ya mtoto wa Kiume na Wakike.

Katika uamuzi huo, amesema kuwa mahakama ya rufaa inaona watoto wote ni sawa bila kuangalia mtoto wa Kiume ama Wakike.

“Hauwezi
kusema ndoa itampa ulinzi mtoto wa Kike wakati huko ndio kwenye
manyanyaso, anaweza kupata mimba za utotoni. Kama mtoto hawezi kupiga
kura na hawezi kuingia katika mkataba wowote, kwanini aingie kwenye
mkataba wa ndoa na aolewe,”

Amesema
kuwa Mahakama ya Rufani inakubaliana na Mahakama Kuu ya kutaka
kubadilishwa kwa kipengele cha 13 cha Katiba ambacho kinasema (Mtoto wa
Kiume awe na 18 ili aweze kuoa na mtoto wa kike anaweza kuolewa chini ya
miaka 18).

Pia
Kifungu cha 17 (Kinatoa namna ambayo mzazi ama mlezi anaweza kutoa
ridhaa ya mtoto kuolewa), vifungu ambavyo vinakiuka Katiba na havina
mashiko.

“Serikali ifate maelezo ya Mahakama Kuu ya kubadilisha sheria hizo,” amesema.

Julai
8, 2016 Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jopo la majaji watatu
wakiongozwa na Shaban Lila ilibatilisha vifungu cha Sheria ya Ndoa
kinachoruhusu ndoa za utotoni.

Kutokana
na uamuzi huo, Serikali ya Tanzania ilikata rufaa ambapo miongoni mwa
sababu zao ni kwamba wanalinda watoto dhidi ya ngono na kupata watoto
nje ya ndoa.

Kesi
ya sheria ya Ndoa za Utotoni ilifunguliwa na Mwanaharakati wa Haki za
Binadamu na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana
Initiative, linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto wa kike ya
kusoma, Rebeca Gyumi.