Uchumi wa afrika kuporomoka kutokana na covid-19

 “Uchumi wa Afrika unaweza kupoteza kati ya dola bilioni 90 na 200
mwaka 2020”

Na Mwandishi Wetu, Arusha

TANGU kulipolipuka kwa ugonjwa wa mapafu maarufu kama corona
(COVID -19), huko katika mji wa Huan katika jamhuri ya watu wa China na baadae
kusambaa katika nchi zingine duniani, idadi kubwa ya watu wameshafariki na
wengine wameendelea kufariki kila uchao kutokana na madhara ya ugonjwa huo.

Licha ya maafa yanayoendelea kutokea tiba ya Corona bado haijaweza
kupatikana ijapokuwa matumaini yameanza kuonekana katika chanjo kadhaa ambazo
zimeweza kugunduliwa na Mataifa mbalimbali duniani ikiwemo iliyogunduliwa hivi
karibuni na wataalamu katika nchi ya Uingereza.


Nchi hiyo baada ya kugundua chanjo hiyo na kuifanyia utafiti wa
kina, jumanne wiki hii Disemba 8, 2020 ilianza kuwapatia wananchi wake na
baadae utaandaliwa utaratibu wa kuweza kuisambaza katika nchi zingine duniani.

Wakati wataalam wakiendelea na upatikanaji wa suluhu ya uhakika ya
kutibia ugonjwa wa Corona, uchumi wa nchi nyingi barani Afrika unaelezwa
kuendelea kuporomoka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinaelezwa
kusababishwa na ugonjwa wa Corona.

Nchini Tanzania, licha ya ugonjwa wa Corona kutokuwepo kama mamlaka
za Kiserikali zinavyoeleza, madhara yake ni makubwa kwa mustakabali wa uchumi
wa nchi lakini pia kwa mwananchi mmoja mmoja.

Uchunguzi unaonyesha kuwa ugonjwa wa corona umesababisha kampuni
nyingi kufunga uzalishaji na zingine kulazimika kupunguza wafanyakazi na hivyo
tatizo la ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likisumbua vichwa vya watawala wetu
kwa namna ya kukabiliana nalo kuendelea kuongezeka kwa kasi kubwa.

Mbali ya Tanzania, bara zima la Afrika limekumbwa na sintofahamu ya
namna ya kukabiliana na matokeo ya ugonjwa wa Corona katika nyanja ya kiuchumi
kufuatia kupungua kwa uzalishaji kwa asilimia kubwa.

Sekta ya viwanda ambayo ndio kiungo cha kutoa ajira imeendelea
kudidimia katika nchi nyingi barani humo na kuhatarisha uchumi wa Serikali
lakini pia uchumi wa mtu mmoja mmoja katika kujipatia mahitaji yake ya msingi.

Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni, uchumi wa Afrika
unaelezwa kuweza kupoteza kati ya dola za kimarekani Bilioni 90 hadi bilioni
200 kwa mwaka 2020 kutokana na madhara ya ugonjwa wa Corona kulingana na utafiti
uliopewa jina la Tackling COVID-19 barani Afrika, ambao ulitolewa wiki hii na wataalam
wa kampuni ya Kimataifa ya ukaguzi ya McKinsey & Company.

Imegunduliwa kuwa hasara hizi zimetokana na kupungua kwa matumizi
ya kibinafsi na marufuku ya kusafiri kuenea barani Afrika, na vile vile
kuahirishwa kwa uwekezaji kutoka mataifa ya nje.

Wakati
athari za uchumi zikiendelea huku bei ya mafuta ikishangaza wengi barani Afrika
kwa kuendelea kupana kila uchao,hali hii ya kiuchumi itajidhihirisha kwa njia
tofauti katika mataifa mengine kama vile Nigeria, Afrika Kusini, Kenya na
Tanzania.



Ripoti hiyo imeshauri Serikali za Kiafrika na washirika wa maendeleo ikiwemo
mashirika ya kimataifa kufanya utafiti wa njia mbadala za kupata suluhisho kama
vile kuwa na mipango ya maendeleo ya kiuchumi.



Aidha ripoti hiyo ilipendekeza pia “Mfuko wa Ushirikiano wa Afrika”
ambao unaruhusu wafanyabiashara na watu kuchangia juhudi za misaada kwa
“biashara zilizo hatarini zaidi.” Ili kunusuru uchumi katika nchi
hizo.


Zaidi ya hayo, mfuko wa sekta binafsi unaweza kuanzishwa kwaajili ya kutoa
misaada, mikopo ili “kusaidia biashara na kupunguza upotezaji wa
kazi.” Jambo ambalo linahitaji tafakuri na busara ya hali ya juu.