Uhasibu Arusha wafanikiwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi walemavu

Egidia Vedasto,

APC Media, Arusha.

Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha kimefanikiwa kuweka mazingira wezeshi na jumuishi kwa Wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum ambayo ni walimu wabobezi katika masuala ya saikolojia na ushauri.

Pia mazingira mengine ni miundombinu ya vyoo na madarasa, vifaa vya kujifunzia na kuwaongezea muda wakati wa kufanya mitihani wanafunzi wenye uhitaji maalum ili kuendana na sera ya kidunia katika mikakati ya kuhakikisha watu wote wanapata elimu bila kikwazo chochote.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu na Mahitaji Maalum Duniani katika chuo hicho, Naibu Mkuu wa Chuo, Ushauri wa Kitaalam Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha Profesa Epaphra Manamba amesema katika kuadhimisha na kusherehekea siku hiyo muhimu chuo kimeanzisha rasmi sera ya watu wenye ulemavu, kuwasajili na kutambua changamoto zao.

Wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum katika Chuo cha Uhasibu Arusha, aliyekaa kwenye kitimwendo ni Emmnuel Kimambo

” Pia tumeanzisha dawati na kurekebisha mitaala na kuwajumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalum lengo likiwa ni wote kwa pamoja kupata elimu na kutimiza ndoto zao” amesema.

Aidha ameitaka jamii kuondoa fikra na imani potofu juu ya watu wenye ulemavu, bali washirikishwe katika kufanya maamuzi na jamii itambue kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa ya kuibadilisha maisha, kujitegemea na kuongeza pato la taifa.

“Katika siasa kuna viongozi wengi wenye ulemavu na wanafanya vizuri, wamekuwa chachu ya maendeleo kwa taifa na wanaaminika, lakini si hivyo tu bali hata hapa chuoni tuna wanafunzi hawawezi kutembea vizuri lakini wanafanya vizuri darasani,” amesema na kuongeza:

” Wengine hawawezi kuongea vizuri nao wana bidii na matokeo yao ni mazuri, niwasihi wazazi na jamii yote, kuweni na imani njema kwa watu wenye mahitaji maalum maana binadamu wote ni sawa na kila mtu ana mchango wake tusibaguane” amefafanua Profesa Manamba.

Kwa upande wake Dkt Lwimiko Sanga anayefanya kazi katika chuo kikuu cha Dar es salaam shule ya elimu, masuala ya saikolojia ya jamii na masuala ya watu wenye ulemavu, ambaye amekuwa muwezeshaji kwa siku hii, ameeleza kuwa ulemavu upo iwe kwa wanyama, binadamu au mimea na unaweza kutokea muda wowote bila kutarajiwa, hivyo ni vema kutowanyanyapaa na kuwabeza watu wenye ulemavu.

Dkt Lwimiko Sanga anayefanya kazi katika chuo kikuu cha Dar es salaam shule ya elimu, masuala ya saikolojia ya jamii na masuala ya watu wenye ulemavu, ndiye amekuwa muwezeshaji na mtoa mada mbalimbali zinazohusiana na watu wenye Ulemavu

Ameeleza kwamba, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe watu hawa wanapata mahitaji yao ya msingi na huduma za kijamii kama elimu, afya kusikilizwa na watoto kushiriki michezo

“Sisi katika chuo chetu tumekuwa mfano mzuri wa kutoa elimu jumuishi kwa kuangalia mahitaji ya kila kundi, elimu hii ilianza kutolewa chuoni mwaka 1978 tukianza na wanafunzi 2, na sasa wamekuwa wengi na kuna miundo mbinu wezeshi vifaa na walimu waliobobea ameongeza,

“Kwa mfano kipindi cha mitihani tumekuwa tukiwaongezea muda wa dakika 15 kwa kila saa moja kwa wanafunzi wenye (speed) ndogo ya kuandika, wasioweza kuongea vizuri na hata kusikia hii yote ni kutoa elimu kwa wote katika mazingira rafiki” amesema Dkt. Sanga.

Vile vile Mkuu wa Idara ya Elimu, Mratibu wa Masuala ya Elimu Jumuishi na Elimu Maalum Katika Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha Mwalimu Godwin Ulio amesema kwa sasa chuo hicho kina wanafunzi wenye mahitaji maalumu zaidi ya 50, wakiwemo wasioona, wasiosikia, walemavu wa ngozi, walemavu wa miguu na wasioweza kuongea vizuri.

Hata hivyo ameeleza namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na taasisi mbalimbali katika kutengeneza sera ambayo tayari imepitishwa na Kamishna kwa lengo la kusimamia mambo yote yanayohusu watu wenye ulemavu ikiwemo kuboresha mazingira ya miundombinu, ambapo kwa ufadhili wa mkopo wa Benki ya Dunia majengo yanaendelea kujengwa chuoni hapo yenye miundombinu rafiki.

“Tumekuwa tukiwafundisha wanafunzi wetu upendo, kusaidiana na kushirikiana, hivyo hakuna wasiwasi kwa mwanafunzi yeyote mwenye mahitaji maalumu atakayetaka kujiunga na chuo hiki”amefafanua Mwalimu Ulio.

Mmoja wa watu wenye ulemavu Emmanuel Kimambo amesema wazazi ndio sababu pekee ya kumfanya mtoto mwenye ulemavu kufikia malengo yake au kushindwa kutimiza ndoto zake kutokana na suala hilo kuwa ndani ya uwezo wao.

“Mfano mimi niliambiwa, nilizaliwa na kukua vizuri, lakini nilipofikisha miaka mitatu niliugua na kushindwa kutembea, safari yangu ya ulemavu ilianzia hapo, kwa sababu wazazi wangu waliona umuhimu natakiwa kupata elimu walinipeleka shule nikasoma hadi chuo, na sasa mimi ni fundi wa umeme na masuala ya mitandao, naendesha maisha yangu na kusaidia wengine, natoa wito kwa wazazi na walezi msifiche watoto ndani, huwezi jua unamficha kiongozi wa baadae au mtalaam katika masuala muhimu” amesema Kimambo.

Katika namna hiyo hiyo Sayuni Msuya mwanafunzi wa chuo hicho wa mwaka wa pili katika masomo ya benki na fedha
amesema anafurahia vile alivyo na anaamini atatimiza malengo yake.

“Mimi ni mlemavu wa miguu lakini nashukuru uongozi wa chuo changu, na wanafunzi wenzangu wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa, sina wasiwasi naamini nitakuwa vile nataka” amezungumza Sayuni.

Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu “Kukuza Uongozi wa Watu Wenye Ulemavu Kwa Mustakabali Shirikishi na Endelevu”.

Naibu Mkuu wa Chuo na Mshauri wa Kitaalam Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (AII) Profesa Epaphra Manamba akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum chuoni hapo